Watu 4,866 walipwa kifuta jasho Sh1.1 bilioni

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jijini Dodoma leo Juni 2, 2023.

Muktasari:

  • Wizara ya Maliasili na Utalii imelipa jumla ya Sh1.13 bilioni kama kifuta machozi na kifuta jasho kwa watu waliopatwa na madhira yaliyotokana na wanyama wakali.

Dodoma. Wizara ya Maliasili na Utalii imelipa jumla ya Sh1.13 bilioni kama kifuta machozi na kifuta jasho kwa watu waliopatwa na madhira yaliyotokana na wanyama wakali.

Waziri wa Malisili na Utalii, Mohamed Mchengerwa alitoa kauli leo Ijumaa Juni 2, 2023 wakati akiwasilisha hotuba ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Hata hivyo Waziri Mchengerwa amesema duniani kote, imebaki Tanzania ndiyo nchi inayolipa fedha kwa watu waliokutwa na madhira hayo, huku akiahidi kuwa wanajiandaa kufanya marekebisho ya sheria ili kuongeza kiwango cha malipo.

Wabunge wamekuwa wakilalamikia viwango ambavyo hulipwa na Serikali kwa mtu anayeuawa, kujeruhiwa au kuharibiwa mazao kutokana na wanyama wakali.

Leo Mchengerwa amesema fedha hizo zimelipwa kwa watu 4,866 kutoka wilaya 36 nchini kote lakini akawaambia wabunge kuwa, Serikali imeshatoa fedha kwa Wizara kwa ajili ya malipo kwa wengine.