Makamba akiri changamoto za umeme, ataja mkakati

Waziri wa Nishati, January Makamba akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024 leo Jumatano Mei, 31, 2023 jijini Dodoma.  Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Wizara ya Nishati imesema rekodi ya mahitaji ya nishati ya umeme nchini imevunjwa mara nane katika mwaka unaomalizika Juni mwaka huu, huku kiwango cha uzalishaji kikielemewa na kasi ya ongezeko la mahitaji ya nishati hiyo hatua inayotishia ukuaji wa sekta na maendeleo ya kiuchumi.

Dar es Salaam. Wizara ya Nishati imesema rekodi ya mahitaji ya nishati ya umeme nchini imevunjwa mara nane katika mwaka unaomalizika Juni mwaka huu huku kiwango cha uzalishaji kikielemewa na kasi ya ongezeko la mahitaji ya nishati hiyo hatua inayotishia ukuaji wa sekta na maendeleo ya kiuchumi.

 Waziri wa Nishati January Makamba ametoa kauli hiyo bungeni leo  Mei 31, 2023 wakati akiwasilisha taarifa fupi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 kuhusu mwenendo wa nishati duniani, utekelezaji wa shughuli za wizara, mchango wake kimaendeleo na mpango kwa mwaka ujao.

“Rekodi hiyo siyo jambo hili la kawaida katika rekodi ya mahitaji ya umeme nchini. Pia kuna upungufu wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme, baadhi ni chakavu, mingine imezidiwa na matumizi ikatumika tofauti na ilivyokusudiwa,”amesema Makamba.

Hata hivyo amesema mipango ya wizara hiyo ni . Kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 1,872 mwaka 2023 hadi 5,810 mwaka 2025/26 ili kukidhi mahitaji hayo kupitia utekelezaji wa miradi ya umeme wa nishati wa vyanzo mbalimbali ikiwamo nishati jadidifu.


Aidha, kuongeza njia na idadi ya njia za kusafirisha umeme, kutoka Kilometa 6,110.28 kwa sasa hadi kilometa 10670.65 mwaka 2025/26. Njia za usambazaji umeme ni kuongeza urefu kutoka umbali wa kilometa 154,567 mwaka 2021/22 hadi kilometa 226, 302 mwaka 2025/26.

Uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka kwa asilimia 10.5 na kufikia MW 1,872.05 ikilinganishwa na MW 1,694.55 zilizokuwepo mwaka 2021/22.

Ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP), MW 2,115 umefikia asilimia 86.89 ikilinganishwa na asilimia 60.22 za mwezi Aprili, 2022.

 Hadi kufikia Mei 23, 2023 kina cha maji ya bwawa hilo kilikuwa kimefikia mita 160.51 kutoka usawa wa bahari ambapo ili kuweza kuzalisha umeme, kiwango cha chini cha maji kinatakiwa kufikia mita 163 kutoka usawa wa bahari.


Mradi wa Kinyerezi 1 Extension wa megawati 185 umekamilika, mitambo yote minne ikiwashwa na kuanza kuchangia katika Gridi ya Taifa.

Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Rusumo megawati 80 umefikia asilimia 99 na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Makamba amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa fupi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 kuhusu mwenendo wa nishati duniani, utekelezaji wa shughuli za wizara, mchango wake kimaendeleo, na mpango kwa mwaka ujao.