Mchengerwa aitaka Tanapa kushuka migogoro Hifadhi ya Serengeti

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa.

Muktasari:

  • Katika ziara hiyo, Waziri Mchengerwa ameambatana Naibu Katibu Mkuu, Anderson Mutatembwa, Kamishna wa Tanapa, William Mwakilema na kupokewa na uongozi wa Mkoa wa Mara, uongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amekutana na kufanya vikao na wananchi wa vijiji vyenye migogoro ya mipaka na Hifadhi ya Serengeti na kuutaka uongozi wa Hifadhi ya Taifa (Tanapa) kuimarisha programu za ujirani mwema na kuwashirikisha wananchi wanaozunguka hifadhi wakati wa kupanga mipango yao.

 Amekwenda mbali zaidi na kutaka wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uhifadhi wa raslimali hizo na kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Akizungumza leo Mei 28, alipofanya ziara katika Wilaya ya Tarime na kufanya mikutano kwenye vijiji vyote vinavyozunguka Hifadhi ya Serengeti vilivyokuwa na migogoro na mipaka, Waziri Mchengerwa ameutaka uongozi wa Tanapa kushuka chini kwa wananchi ambao ndio wahifadhi wa kwanza na kuzungumza nao.

Awali wananchi hao walimueleza waziri kutoshirikishwa ipasavyo kwenye mipango ya uhifadhi jambo ambalo likifanyika litasaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima.

Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard amesema  kuwa wananchi wa kata yake wapo tayari kushirikiana na Serikali kwenye  kila jambo endapo uongozi wa hifadhi utawashirikisha.


“Waziri nakuhakikishia kuwa leo tutapata usingizi, kwani tunaamini umetumwa na Rais wetu kuja kutujengea mahusiano mazuri, na sisi hiki ndicho  tulichokuwa tunakikosa kwa muda saaa,” amesema Diwani Richard.

Kwenye Kijiji cha Karakatonga wilayani Tarime, waziri Mchengerwa aliwasikiliza wananchi na kuutaka uongozi wa Tanapa kushuka  chini na kusikiliza kero zao kwani wananchi ndio wahifadhi wa kwanza.

Akiwa kwenye Kijiji cha Kegonga, Mchengerwa ametoa wito  kwa wananchi  kushirikiana na uongozi wa Serikali na kuacha migomo ambayo ni moja ya vichocheo vya migogoro.

“Wanapokuja  viongozi wa Serikali ili kujadili mpango wa matumizi bora ya ardhi msikatae, wasikilizeni na kushauri tufanye nini," amesema Mchengerwa.

Aidha amewataka wananchi hao kutambua wahifadhi  ni sehemu ya  jamii yao kwani baadhi ya watumishi wa hifadhi ni sehemu ya familia zao na watoto wao.