Mchengerwa apokea mawakala 40 wa utalii kutoka China

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa akizungumzia ujio wa mawakala wa utalii kutoka China.

Muktasari:

  • Wageni hao 40 ni kutoka makampuni makubwa ya habari na utalii nchini China ambao wamealikwa na Serikali kuja kutembelea vivutio vya hapa nchini na kwenda kuvitangaza kwa ajili ya kuwaleta watalii wengi kutoka Taifa lao.

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amepokea ugeni wa mawakala, waandishi wa habari na wawekezaji wa sekta ya utalii 40 kutoka nchini China waliofika hapa kwaajili ya kutembelea vivutio mbali mbali nchini.

 Akipokea ugeni huo, Mchengerwa alisema kuwa wageni hao ni kutoka makampuni makubwa ya utalii nchini China ambao wamekuwa wakisafirisha zaidi ya watalii milioni 40 kwa mwaka kwenda maeneo mbali mbali duniani kutalii.

"Tumewaleta hapa kuwaonyesha na sisi vivutio vyetu tulivyonavyo wakavitangaze na kutuletea watalii zaidi hivyo watu wanaofanya kazi ya kuongoza watalii chukueni hii fursa tuliyofungua China ikiwemo safari zetu za ndege kuhakikisha mnabuni bidhaa mpya za utalii na kutangaza zilizopo," amesema.

Ugeni huo ni matokeo ya utangazaji wa bidhaa za utalii nchini iliyofanywa na Rais Samia Suluhu kupitia filamu ya royal tour hali iliyofungua soko la utalii nchini China.

Alisema kwa miaka mingi kazi ya kutangaza utalii waliachiwa sekta binafsi lakini kwa sasa Serikali imeingia kati kuongeza nguvu ambapo wanaandaa mkakati mpya utakaosaidia kutoa muongozo wa mambo muhimu ya kuzingatia.

"Jitihada hizi zimeanza kuzaa matunda kwani tayari tumeingiza zaidi ya watalii tofautitofauti milioni 1.5 na mwaka 2021 tuliingiza watalii wasiozidi milioni 900," alisema Mchengerwa na kuongeza.

"Hofu yangu kwa sasa ni uchacche wa hoteli za kulala watalii wetu, wasije kukosa malazi ikawa aibu kwetu naomba wawekezaji tumieni fursa hii kuzijenga na Serikali itawapa sapoti zote,"amesema.

Mchengerwa alitoa onyo kwa baadhi ya watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara yake wanaojihusisha kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuweka urasimu kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye Sekta ya utalii.

"Nimeanza kuchukua hatua na nitaendelea kushusha rungu kwa watendaji watakaoshinda kwenda na kasi hii ya kufanikisha maendeleo ya utalii nchini ikiwemo kukwamisha wawekezaji, kwa maslahi yao binafsi au kuendekeza vitendo vya rushwa hatutavumiliana," amesema.

Mkaguzi mkuu wa ndani Benk ya NMB Benedict Baragumwa alisema kuwa waliamua kushirikiana na taasisi za serikali kuhakikisha watalii hao wanafika nchini kwa ajili ya kuongeza pato la taifa lakini pia kuitangaza benki.

"Sisi tumefungua matawi rafiki China na hapa wamekuja kuna matawi kwenye vituo vya utalii wataweza kupata huduma zote za kifedha kupitia benki yetu na tumejipanga kwa ajili yao," amesema.

Nae mkurugenzi wa Bodi ya utalii 'TTB' Damas Mfugale alisema kuwa ujio wa mawakala hao wakubwa wa utalii nchini ni mafanikio ya mikakati waliyojiwekea ya kufungua masoko katika mataifa yenye watalii wengi duniani.

"Tuko kwenye mazungumzo na mabalozi hasa nchi zetu za kimkakati kwa ajili ya kuhakikisha nchi inatembelewa na watu wengi zaidi katika malengo ya kufikisha watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025," amesema.