Tanapa yasaini mikataba nane ya Sh157.29 bilioni

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, William Mwakilema, (wa pili kulia) akisaini moja ya mikataba nane iliyo chini ya  REGROW na mkandarasi kampuni ya Badr East Africa enterprises limited leo Jumatatu Aprili 17, 2023 jijini Arusha.

Muktasari:

  • Tanapa imesaini mikataba hiyo  iliyoko chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) inayolenga kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza sekta ya utalii katika mikoa ya Kusini.

Arusha. Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), imesaini jumla ya mikataba nane yenye thamani ya Sh157.29 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu iliyoko chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

Utiwaji wa saini umefanyika leo Aprili 17, 2023 jijini Arusha baina ya shirika hilo la Tanapa na wakandarasi watakaotekeleza ambapo umeshuhudiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa.

Aidha mikataba iliyosainiwa imegawanyika katika makundi mawili ikiwemo mikataba minne ya ujenzi wa majengo pamoja na mikataba minne ya ujenzi wa viwanja vya ndege ambayo itatekelezwa katika hifadhi nne za Ruaha, Mikumi Udzungwa na Nyerere na Msitu wa Asili wa Kilombero chini ya TFS .

Akizungumza katika zoezi hilo, Waziri Mchengerwa amewataka wakandarasi hao kufanya kazi kwa muda walioahidi kwani hakutakuwa na muda wa ziada utakaoongezwa zaidi watachukuliwa hatua za kisheria.

"Miradi hii inatekelezwa kwa mkopo kutoka benki ya dunia na umeshacheleweshwa kwa zaidi ya miaka mitano tangu mwaka 2017 uliyotakiwa kuanza hivyo basi nendeni mkatendee haki fedha hizi za wananchi kwa manufaa iliyokusudiwa ya kuongeza pato la serikali na mwananchi mmoja mmoja," amesema.

Mchengerwa pia aliwataka watendaji wa wizara yake kuusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ili kukamilika kwa wakati kwa kiwango bora huku akiwatahadharisha uwajibikaji katika dosari yoyote itakayojitokeza.

Alisema kwenye mikataba ya ujenzi wa viwanja inatarajiwa viwanja sita vya ndege kujengwa ambapo viwanja vitatu vya ndege vitajengwa hifadhi ya Ruaha, viwanja viwili Hifadhi ya Mikumi na Hifadhi ya Nyerere kitajengwa kiwanja kimoja cha ndege.

Aidha alisema katika Hifadhi ya Udzungwa kutajengwa njia ya juu ya watalii inayokadiriwa kuwa na kilomita moja ambayo inatarajiwa kuwa miongoni mwa njia ndefu zaidi Afrika Mashariki na hata kusini mwa Afrika itakapokamilika.

"Miundombinu mingine ni majengo ya utalii, mageti, vituo vya habari, nyumba za watalii, hosteli vituo vya askari pamoja na maeneo ya kupumzikia yatajengwa ili kuhakikisha watalii wanafurahia wanapotembelea katika maeneo hayo yote hii ni kuboresha huduma za watalii na kuongeza mapato kwani utajiri wa rasilimali tulizonazo haiakisi kiasi cha mapato tunayoingiza," amesema.

Naye katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi amesema kuwa Mradi REGROW ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza Sekta ya Utalii katika Mikoa ya Kusini lakini ulicheleweshwa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu.

"Mradi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia lakini kuna baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi walichelewesha sasa niseme tumeanza upya na watakaobainika kuingiza ucheleweshaji tena tutawatafutia mahala salama ya kuishi ili watupishe," amesema.

Awali kamishna wa Uhifadhi Tanapa, William Mwakilema aliishukuru serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii kwa kuwezesha mradi huo na kuichagua Tanapa kuwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza na kunufaika nao.

Alisema mradi huo ukikamilika unalenga kuimarisha utoaji wa huduma za utalii  na kuongeza kipato kwa wananchi waliopo kusini mwa Tanzania.

Alisema Tanapa inakabiliwa na changamoto za ujangili, ubovu wa miundo mbinu hasa barabara na viwanja vya ndege na changamoto hivyo mradi huo unakwenda  kutatua changamoto hizo.