Serikali kutoa kauli sakata la tozo leo

Serikali kutoa kauli sakata la tozo leo

Muktasari:

Serikali ya Tanzania leo Jumanne, Septemba 20, 2022, Bungeni jijini Dodoma itatoa majibu ya malalamiko ya Watanzania kuhusu tozo za miamala ya kieletroniki mara baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni.

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba leo Jumanne, Septemba 20, 2022 atatoa majibu ya malalamiko ya Watanzania kuhusu tozo za miamala ya kielektroniki.

“Leo sasa nitatoa majibu kuhusu lile swali lako ambalo umekuwa ukiniuliza (tozo za miamala ya kieletroniki),” amesema Dk Mwigulu.

Waziri huyo amesema hayo leo asubuhi katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma wakati akiingia bungeni.

Kwa mujibu wa orodha ya shughuli za Bunge leo, inaonyesha kutakuwa na kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Bunge, kauli za mawaziri hazijadiliwi na wabunge.

Jana Jumatatu, akizungumza na Mwananchi, Dk Mwigulu alisema siku nyingi angetangaza uamuzi wa Serikali kuhusu malalamiko ya tozo ya kielektroniki.

Serikali kutoa kauli sakata la tozo leo

Septemba 2022, Dk Mwigulu alisema Serikali imeunda timu kwa ajili ya kufanyia kazi malalamiko ya tozo katika miamala ya kielektroniki.

“Timu hiyo iliyoundwa itakuja na njia rafiki ya ukusanyaji wa mapato,” alisema Dk Mwigulu alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara Wilayani Tarime mkoani Mara.

Dk Mwigulu alisema wataalam wa wizara yake wanafanyia kazi maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi (CCM), kwamba muda si mrefu Serikali itakuja na majawabu ya baada ya kufanya marekebisho kadhaa ya kuleta unafuu.

Hata hiyo, imekuja baada ya mjadala mpana kuhusu tozo za miamala ya kielektroniki, wananchi na wadau wengine wamekuwa wakipinga baadhi ya tozo zilizoanzishwa na Serikali.

Baadhi ya wasomi, wanasiasa na wananchi kutaka tozo hizo ama zipunguzwe au zifutwe kabisa, wakisema zinawaongezea ugumu wa maisha unaosababishwa na kupanda kwa bei huku zikitishia mzunguko wa fedha kwenye sekta rasmi.

Aidha, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ilielekeza Serikali kuchukua ushauri wa wananchi kuhusu tozo sambamba na kujielekeza katika kubana matumizi ya serikali na kutanua wigo wa kodi.

Tozo hizo zilianza kutumika Julai Mosi, 2022, baada ya Serikali kutoa Kanuni za Sheria ya Mifumo ya Kitaifa ya Malipo (Tozo za Miamala ya kieletroni).