Serikali kutumia gesi asilia kupunguza uhaba wa umeme

Muktasari:

  • Serikali imesema ili kukabailiana na changamoto ya umeme nchini wataangalia ni namna gani watakavyojikita kwenye vyanzo ambavyo ni rafiki kwa mazingira ikiwemo matumizi ya gesi asilia.

Dodoma. Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuboresha mifumo ya matumizi ya gesi asilia kwenye uzalishaji wa umeme nchini badala ya kutegemea chanzo cha maji pekee.

Hata hivyo, chanzo cha nishati utajikita zaidi kwenye vyanzo rafiki vitakavyochangia kwenye utunzaji wa mazingira vinavyosababisha mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yameelezwa leo Novemba 9, 2023 na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga wakati akizungumza kwenye Jukwaa la uziduaji la mwaka 2023 lenye lengo la kujadili na kufanikisha mhamo wa nishati na maendeleo endelevu katika sekta ya uziduaji Tanzania.

Aidha Kapinga amesema licha ya kuwepo na vyanzo hivyo vinavyolinda mazingira lakini bado vina changamoto ya mikataba inayozuia masuala ya matumizi yake.

Amesema Serikali itaangazia ni kwa namna gani watatumia vyanzo hivyo huku wakikubaliana na mikataba ya Kimataifa na vipi Watanzania watanufaika na matumizi ya rasilimali za kuzalisha umeme.


Kapinga amesema Serikali itaendelea kuboresha matumizi ya gesi kwenye uzalishaji wa umeme na hata hivi karibuni wameboresha vyanzo vikuu vya gesi vikiwemo visima vya Songosongo na madiba Ili kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Hakirasilimali, Adam Anthony amesema kwenye jukwaa hilo wadau pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa watapata faida ya kujifunza haki zao katika kunufaika na sekta ya uziduaji ambayo inatajwa kuharibu vyanzo vya nishati.

Amesema wakati wa utekelezaji wa mhamo wa Serikali na makampuni ione dhamira ya kurudisha kwa wananchi hususan wanaoishi kwenye maeneo hayo.

“Kwa mfano ukizungumzia migodi ya dhahabu ni vema vijiji vinavyozunguka mgodi huo vikanufaika kwa miradi tofauti ikiwemo ajira na afya, hii inasaida kuipa uhuru Kampuni kufanya kazi bila ya kuwa na mgogoro na jamii,”amesema Anthony.

Bonny Motto amesema Serikali na makampuni ione namna ya kuheshimu wananchi wa Tanzania ambao wanafanya tafiti na wao kwenda kuwekeza kwenye maeneo hayo.