Viongozi wa dini: Tutunze mazingira kulinda JNHPP

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na viongozi wa dini Jumuiya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki (TEC), waliotembelea mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere.

Muktasari:

  • Viongozi wa dini watembelea mradi wa kufua umeme Bwawa la Julius Nyerere na kuhimiza utunzaji na uhifadhi wa mazingira, wakisema huo utakuwa ujumbe wao kwa waumini.

Pwani. Viongozi wa dini wameiomba Serikali kwa kushirikiana na wananchi kutunza mazingira ili kuulinda na kuufanya mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) uwe endelevu na kutoa matunda yanayotakiwa.

 Viongozi hao kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), jana Jumanne, Julai 11,2023 wamefanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo wakiongozwa na Waziri wa Nishati, January Makamba.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Makamba amesema kutokana na mvua kunyesha kwa kiwango cha kuridhisha bwawa hilo hivi sasa linaweza kuzalisha umeme kama mashine zingekuwa zimekamilika kufungwa.

Alisema mradi huo unaogharimu takribani Sh6.5 trilioni utakaozalisha megawati 2,115 unatarajia kuanza majaribio ya kufua umeme Februari mwakani na kuwa suluhisho la uhaba wa umeme.

“Haya mambo tunayoyaona hivi sasa yanatokana na utunzaji wa mazingira na sisi tumedhamiria kuyatunza kwa kushirikiana na wenzetu, tangu awali shughuli zilizofanyika hapa zilizingatia mazingira. Tunashukuru Mungu ujio wa viongozi wetu wa dini walioumbea mradi huu sambamba na Rais (Samia Suluhu Hassan),” alisema.

Waziri Makamba alisema kuna wakati walilazimika kutumia helikopta kuwatoa wanyama waliokuwa wamezingirwa na maji baada ya mradi kuanza.

“Kimsingi tangu awali tulichukua kila hatua kuhakikisha mazingira yanalindwa hivyo tunaamini tukishirikiana kuyatunza tunanufaika zaidi na huu mradi ambao ni wa kihistoria,” alisema.

Akizungumzia ziara hiyo, mwakilishi CCT, Askofu Maimbo Mndolwa alisema wanaamini bila vyanzo vya maji kutunzwa hautatoa manufaa yaliyotarajiwa.

“Shughuli za kilimo, ufugaji na nyingine zikifanyika kwenye vyanzo vya maji bwawa hili haliwezi kupata maji ya kutosha hivyo hatutapata ufanisi, tusipopata ufanisi maana yake fedha zetu zitakuwa zimepotea lakini hatutaondoka kwenye uhaba wa umeme,” alisema.

Mndolwa ambaye ni Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Tanga amesema wananchi wanapaswa kutunza mazingira ili nayo yawatunze na kuwasaidaia katika maisha yao ya kila siku.

Mwakilishi huyo wa CCT ambaye pia Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, amesema bwawa hilo sio tu litakuwa msaada kwa Watanzania lakini litawezesha mataifa ya jirani kunufaika.

Naye, Mwakilishi wa TEC, Askofu Lazarus Msimbe wa Jimbo Katoliki la Morogoro, amesema maendeleo ya nchi yanahitaji ushirikiano na kuthamini kila kinachofanywa na viongozi ili kuwapa moyo.

Amesema maendeleo ya Tanzania yanahitaji uwepo wa uhakika wa umeme hivyo mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo na kutatu mgawo wa umeme unaotokea mara kwa mara.

“Jambo la msingi ni kuwa hata sisi sasa tutakuwa na umeme wa ziada hivyo tunaweza kuuza au hata kama watu wana matumizi makubwa hawatakuwa na shaka ya umeme” amesema Askofu Msimbe.

Askofu Msimbe amesema watamuomba Mungu awape nguvu viongozi waendelee kusimamia kikamilifu miradi yote ya kimkakati ili ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha Watanzania.

Hata hivyo, amewataka Watanzania waendelee kuyatunza mazingira kwa faida yao na vizazi vijavyo kama alivyoagiza Mungu.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi wa mradi wa JNHPP, Lutengano Mwandambo amesema hadi  sasa mita za ujazo wa maji katika bwawa hilo limefikia 163.7 kutoka usawa wa bahari hivyo kuwezesha kufanyika kwa uzalishaji.

“Tunaamini mvua zikienda vizuri ndani ya misimu miwili tu, uzalishaji utaanza vizuri na kwakuwa hapa kuna bwawa la kuhifadhji maji tunaamini mradi huu utakuwa na manufaa zaidi kwa nchi yetu” amesema.