Serikali kuwafadhili watakaosoma Tehama Zanzibar

Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda

Muktasari:

  • Serikali kupitia Wizara ya Elimu, imesema baadhi ya wanafunzi watakaopata ufadhili wa masomo ya sayansi (Samia Scholarship), watapelekwa kusoma katika Taasisi ya Teknolojia India (IIT) tawi la Zanzibar linalotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Elimu, imesema baadhi ya wanafunzi watakaopata ufadhili wa masomo ya sayansi (Samia Scholarship), watapelekwa kusoma katika Taasisi ya Teknolojia India (IIT) tawi la Zanzibar linalotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Hayo yamesemwa leo Julai 7, 2023 na Waziri wa Elimu Adolf Mkenda alipomkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa India Subrahmanyam Jaishankar, pale alipotembela tawi la IIT lililopo katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Waziri Mkenda amesema, kuanzia Oktoba mwaka huu, IIT Zanzibar itachukua wanafunzi 50 wa shahada ya kwanza na wengine 25 wa shahada ya pili, na kwamba pia mikopo itatolewa kwa wanafunzi ambao hawatapata ufadhili huo.

Amesema wanafunzi watakaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kidato cha sita, wanatakiwa kuomba ufadhili wa kusoma masomo ya tehama yatakayotolewa na IIT Zanzibar.

"Tungependa kuwapeleka wanafunzi wetu India lakini ni gharama kubwa na kwakuwa shahada hizo sasa zitatolewa nchini, tena kwa kuratibiwa na IIT, hivyo tutawapa ufadhili wa masomo hayo katika vituo vilivyofunguliwa hapa nchini," amesema Mkenda.

Amesema elimu itakayotolewa na taasisi hiyo italingana na ile inayotolewa nchini India na kwamba itasimimamiwa na Seneti ya IIT nchini humo (India) ili kuepuka kuchakachua ubora wa elimu.

Mkenda amesema walishakubalina juu ya vigezo ambavyo vilitakiwa na chuo hicho cha India na kwamba wizara hiyo inayosimamia masuala yote ya elimu nchini, itahakikisha pesa za ufadhili huo zinapatikana.

"Tutaangalia na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba kuona namna gani tutaongeza fedha ili kuhakikisha malengo na azma ya Rais Samia kuanzisha ufadhili huo inatimia.