Serikali, mkandarasi kujadiliana ucheleweshaji reli ya SGR
Muktasari:
Ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilometa 368 unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh4.4 trilioni. Utekelezaji wa mradi huo ulianza Machi, 2023 na unatarajiwa kumalizika ifikapo Januari, 2026.
Tabora. Serikali imepanga kukutana na uongozi wa kampuni ya Yarp Merkez kujadiliana utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendo kasi (SGR) sehemu ya tatu ya Makutupora-Tabora baada ya kubainika kuwa utekelezaji mradi huo uko nyuma kwa asilimia 10.
Akizungumzia leo Oktoba 6, 2023 wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kwa sasa, utekelezaji wa mradi huo uko asilimia 12 kinyume cha mahitaji ya kimkataba yanayoelekeza uwe umefikia asilimia 22.
''Tutakutana na mkandarasi kujadiliana ili kubaini changamoto zinazochelewesha mradi,'' amesema Profesa Mbarawa
Ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilometa 368 unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh4.4 trilioni. Utekelezaji wa mradi huo ulianza Machi, 2023 na unatarajiwa kumalizika ifikapo Januari, 2026.
Akizungumzia hofu kuwa kusuasua kwa mradi huo unatokana na uezo mdogo wa mkandarasi, Waziri Mbarawa amewatoa hofu Watanzania akisema utekelezaji wa miradi mikubwa una taratibu zake zinazolinda pande zote ambazo huangaliwa pindi upande mmoja unaposhindwa kutimiza wajibu.
"Hadi sasa, mkandarasi anaendelea na kazi na tunaendelea kumsimamia; hajashindwa kutekeleza mradi huu," amesema Profesa Mbarawa
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Nchini (TRC), Senzige Kisenge Serikali tayari imemtaka mkandarasi kuwasilisha mpango kazi wake utakaoonyesha namna ya kufidia asilimia 10 iliyochelewa kuhakikisha kazi inafanyika na kukamilika kulingana na mkataba.