Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali, Ndugai wabeba ndoto ya 'house girl'

Muktasari:

 Ndoto ya Mariam Mchiwa kuendelea na elimu ya kidato cha tano, sasa ni dhahiri, huku gazeti la Mwananchi likitajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuifanikisha.


Dodoma/Dar. Ndoto ya Mariam Mchiwa kuendelea na elimu ya kidato cha tano, sasa ni dhahiri, huku gazeti la Mwananchi likitajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuifanikisha.

Binti huyu aliyehitimu kidato cha nne mwaka jana katika Sekondari ya Songambele iliyopo Kongwa mkoani Dodoma na kufaulu kwa daraja la kwanza, alipoteza matumaini ya kuendelea na kidato cha tano kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo.

Hata hivyo, alitafuta cha kufanya ndipo alipoamua kusafiri hadi jijini Dar es Salaam kutafuta ajira ya kufanya na akapata kazi za ndani alizokuwa anafanya kwa dhamira ya kutafuta fedha ambazo angezitumia kujisomesha.

Baada ya uchaguzi wa majina ya kidato kutoka na yeye kuonekana amepangiwa Sekondari ya Wasichana Songea, Mwananchi liliripoti kuhusu changamoto anazopitia binti huyu na uongozi wa Mkoa wa Dodoma na wadau wengine, likiwamo Baraza la Kuu la Waislamu (Bakwata), wamejitokeza kumsaidia kutimiza ndoto yake ya kuendelea na masomo.

Jana uongozi wa Mkoa wa Dodoma ulilishukuru Mwananchi kwa kuibua habari binti huyo anayesubiri kwenda Songea mkoani Ruvuma kuendelea na masomo.

Mbali na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, Sheikh wa mkoa huo, Mustapha Rajabu alisema kama si Mwananchi kuibua habari ya binti huyo isingeonekana mapema na kumsaidia kutimiza malengo.

Viongozi hao walitoa kauli hiyo jana baada ya kumkutanisha Mariamu na wadau waliokubali kumsomesha kuanzia kidato cha tano hadi chuo kikuu.

Mtaka alisema habari za binti huyo zilimfanya aamue kubeba jukumu la kumsomesha yeye na viongozi wenzake mkoani hapo kuhakikisha ndoto yake ya kupata elimu inatimia.

“Tuwashukuru watu wote ambao walifanikisha jambo hili, lakini wadau wetu wa Mwananchi pia karibuni hata tupige picha na binti huyu, mmefanya kazi kubwa,” alisema Mtaka.

Mtaka alisema wadau wanaendelea kujitokeza kumsaidia Mariamu na jana alikabidhiwa Sh650,000 zilizochangwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwanza, Profesa Flora Fabiani aliyetoa Sh200,000, Nyambura Moremi Sh150,000 na Benki ya Equity iliyotoa Sh300,000 huku ikimfungulia akaunti isiyo na makato ya uendeshaji.

Mbali na wadau hao, mkuu huyo wa mkoa alisema kuna watu wengi wanataka kumsaidia Mariam ambaye kwa sasa anaishi nyumbani kwa Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai.

“Kwa sasa tunafanya mpango wa kuwafungulia bima ya afya wazazi wake, baada ya kuona kweli wana hali ngumu kiuchumi, lakini mbunge wao ambaye ni Spika mstaafu Job Ndugai ameshazungumza nao na kuridhia binti akasome na binafsi yeye atabeba majukumu makubwa kwa mtoto huyu kama mwanawe,” alisema Mtaka.

Profesa Fabian wa Chuo Kiku cha Mwanza kilichoahidi kumsomesha binti huyo alisema licha ya uchanga wa chuo chao, jukumu la kuunga mkono wadau kwenye elimu ni lao na wangetamani kufanya hivyo kwa sababu binti huyo amechaguliwa katika masomo ya sayansi ambayo wanapenda kuyadhamini.

Profesa Fabian alisema watakuwa na binti huyo katika gharama zote hadi watakapoona amefika chuo kikuu na kumaliza masomo yake bila kukwama kwa jambo lolote.

Akizungumza mbele ya mkuu wa mkoa, Mariam alisema ndoto yake ni kusoma na kufikia mafanikio ya kwenda kuisaidia familia yake, huku akitamani kuwa muuguzi.

Ametaja sababu za kutaka kazi hiyo kuwa ni kutokana na tatizo la kidonda alichonacho baba yake mzazi alichokipata tangu mwaka 1993, baada ya kufanyiwa upasuaji hivyo anaamini kuna mahali wataalamu walikosea.

“Nataka kuwa muuguzi, na kweli ndoto hiyo ndiyo ninayo siku zote, sababu kubwa ni kitendo alichofanyiwa baba yangu na kwa kuzingatia mimi ndiyo niliyesoma kwetu, basi nije niwasaidie familia na watu wengine,” alisema.