Serikali, Tucta kujadili nyongeza ya mishahara

Muktasari:

Siku moja baada ya kuibuka mjadala kuhusu nyongeza isiyoridhisha ya mshahara kwa watumishi wa umma, Serikali imepanga kukutana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) leo kutolea ufafanuzi suala hilo.


Dar/ Unguja. Siku moja baada ya kuibuka mjadala kuhusu nyongeza isiyoridhisha ya mshahara kwa watumishi wa umma, Serikali imepanga kukutana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) leo kutolea ufafanuzi suala hilo.

Hilo linakuja kutokana na kilio cha wafanyakazi wakilalamikia nyongeza kidogo ya mishahara tofauti na matarajio yao kama ilivyotangazwa Mei 14 mwaka huu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia ombi la ongezeko la mishahara.

Kupitia ukurasa wa Twitter wa Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa jana aliandika, “Ndugu wafanyakazi Julai 26, 2022 Serikali itakutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, ili kuwasikiliza na kutoa ufafanuzi kuhusu nyongeza ya mishahara katika mishahara ya Julai 2022.”

Juzi usiku, Msigwa aliandika, “Ndugu wafanyakazi naomba tutulie. Serikali itatoa ufafanuzi kuhusu nyongeza ya mishahahara iliyotokea katika mishahara ya Julai.”

Kauli ya Msigwa imekuja wakati mitandaoni kukiwa kumesheheni malalamiko ya wafanyakazi na wengine wakituma vibonzo vya kejeli na kuhoji kuhusu nyongeza hiyo ambayo inaonekana kutokidhi matarajio ya baadhi yao.

Katika video aliyoonekana kwenye televisheni ya Azam, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alikiri kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wakilalamikia nyongeza hiyo ya mishahara.

“Taarifa hizi za nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa sekta ya umma tumeipokea na tumeifuatilia, ni kweli haijakaa vizuri na tutalizungumzia suala hilo wiki ijayo tutakapokutana kwenye kikao chetu Dodoma.

“Tunaomba watumishi watulie, tutakaa pamoja na Serikali halafu tutawaambia kwa kiwango gani hatujaridhika,” alisema Nyamhokya.

Wakati huohuo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi jana alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuimarisha masilahi ya wafanyakazi na tayari nyongeza ya mishahara waliyoahidiwa wakati wa sherehe za Mei Mosi, mwaka huu imetekelezwa mwezi huu.

Alisema kwa kipindi hiki ambacho wafanyakazi wanaendelea kupokea nyongeza za mishahara, kila mmoja ataongezwa kulingana na kiwango cha elimu na uzoefu wake kazini.

Hata hivyo, aliwataka wafanyakazi hao kukata rufaa kama hawajaridhika au kama wana wasiwasi na kiwango kilichoongezwa kulingana na vigezo vilivyotajwa.

“Tuliahidi, nadhani mmeanza kuona mambo mazuri huko. Tutaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kuleta ufanisi kiutendaji,” alisema Rais Mwinyi.

Kwa mujibu wa vigezo vilivyotajwa, wafanyakazi hao waliongezwa kati ya Sh20,000 na Sh100,000.