Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali: Utaratibu mikopo ya asilimia 10 bado unafanyiwa kazi 

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

  • Suala la mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu limeibuka kwa mara nyingine bungeni.

Dodoma. Serikali bado inaendelea kufanyia kazi utaratibu wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ambayo ilisitishwa Aprili mwaka huu ili kutafuta utaratibu mwingine wenye ufanisi zaidi.

Aprili 13, 2023 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya mwaka 2023/24 ya ofisi yake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema fedha zilizorejeshwa Aprili mwaka huu hazitakopeshwa tena na zinatakiwa kusubiri utaratibu mwingine kwa kadri itakavyoelekezwa.

Uamuzi huo ulikuja wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwa tayari amesema unaandaliwa utaratibu mzuri wa ukopeshaji wa fedha hizo kupitia mabenki ili kuwasaidia zaidi wahitaji.

Leo Jumatano Novemba Mosi, 2023, hoja hiyo imeibuka bungeni baada ya Mbunge wa Nanyumbu (CCM), Ally Mhata kuhoji ni lini Serikali italeta sheria ya kuruhusu halmashauri kutumia benki kama wakala wa ukopeshaji na ukusanyaji madeni.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange amesema Serikali inatambua ufanisi wa kutumia benki kama wakala wa ukopeshaji na ukusanyaji wa madeni kwa kuzingatia kuwa benki zina miundombinu na utaalamu wa kutoa huduma hizo.

Hata hivyo, amesema ili kutumia benki katika kutekeleza jukumu la mikopo ya asilimia 10, maandalizi na utafiti unapaswa kufanyika ili kuendana na lengo kusudiwa.

Amesema Tamisemi iliunda kamati ya kitaifa ambayo ilichambua na kuandaa mapendekezo ya uendeshaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Aidha, amesema timu imeshakamilisha kazi hiyo na kuwasilisha maoni na mapendekezo ambapo Serikali inaendelea kufanyia kazi na baada ya kukamilisha itatoa utaratibu.

Katika swali la nyongeza, Mhata amehoji Serikali haioni haja ya kuwa na mpango wa dharura wa kutoa mikopo wakati wananchi wanasubiri utaratibu huo mwingine kwa sababu wanauhitaji wa fedha hizo hasa wakati huu wa msimu wa kilimo.

Akijibu Dk Dudange amesema lengo la kusitisha mikopo hiyo ni kuhakikisha kuwa inawafikia walengwa lakini zinatumika kwa tija na kurejeshwa ipasavyo.

Amesema hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa iliyosababisha kusitishwa kwa mikopo hiyo.

“Nimuhakikishie mheshimiwa mbunge kuwa Serikali inaenda nalo jambo hili kwa kasi ili kuhakikisha mikopo inaanza kutolewa kwa wananchi badala ya kuwa na utaratibu wa dharura ambao hautakuwa na tija sana kwa sababu bado utakuwa na mapengo mengi,” amesema.