Serikali ya Tanzania imeajiri wahadhiri 502 ndani ya miaka 10

Muktasari:

Kuanzia mwaka 2008 hadi 2019 Tanzania imeajiri wahadhiri 502 kutoka nje ya nchi hiyo

Dodoma. Kuanzia mwaka 2008 hadi 2019 Tanzania imeajiri wahadhiri 502 kutoka nje ya nchi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Mei 24, 2019 bungeni jijini Dodoma na naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Elimu, na kubainisha kuwa wahadhiri hao wameajiriwa katika vyuo 17.

Mwita amesema katika vyuo hivyo, nane ni vya umma wakati wengine walipata ajira katika vyuo tisa binafsi.

Waitara alikuwa akijibu swali la mbunge wa Nkenge (CCM), Dk Diodorus Kamala  aliyehoji  katika kipindi cha miaka 10 wahadhiri wangapi wameajiriwa katika vyuo vikuu nchini.

Mbunge huyo pia alihoji ni mafanikio gani kitaaluma na kiutafiti yameletwa na wahadhiri hao kutoka nje, kutaka kujua ni kwanini Tanzania isiige nchi nyingine ili kuongeza umri wa kustaafu.

Katika ufafanuzi wake Waitara amesema Serikali inafanya jitihada mbalimbali kuendeleza wataalamu wa ndani ili kupunguza wataalamu wa kigeni ambao hadi sasa wamebaki 151.

Naibu Waziri huyo ametaja mafanikio kutoka kwa wageni hao kuwa ni pamoja na kupata wataalamu wa fani mbalimbali ambazo hazijajitosheleza na kuanzishwa kwa programu mpya katika vyuo mbalimbali.

"Lakini pia umewezesha uanzishwaji wa mashirikiano kati ya vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia na vifaa vya maabara," amesema Waitara.

Hata hivyo, Waitara amekiri kuwepo na upungufu wa wahadhiri katika vyuo mbalimbali lakini akasema Serikali inawasomesha wengine 68 nje ya nchi ili kupunguza upungufu huo.