Serikali ya Tanzania yaeleza faida kukusanya kodi bila kutumia mabavu

Muktasari:
- Msemaji mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa amesema ukusanyaji wa mapato bila kutumia mabavu umeimarisha zaidi ukusanyaji kodi.
Dar es Salaam. Msemaji mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa amesema ukusanyaji wa mapato bila kutumia mabavu umeimarisha zaidi ukusanyaji kodi.
Ameyasema hayo jana Jumamosi Juni 5, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dodoma.
Akitoa mfano wa ukusanyaji wa mapato ambao chanzo cha takwimu zake ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), amesema Januari kabla ya agizo la kuacha kutumia mabavu katika ukusanyaji wa kutolewa malengo yalikuwa ni kukusanya Sh1.68 trilioni na zilizokusanywa ni Sh1.34 trilioni sawa na asilimia 79.8.
Mwezi Februari malengo yalikuwa Sh1.61 trilioni huku kiasi kilichokusanywa kikiwa ni Sh1.33 trilioni.
Amesema ilipofika Machi, 2021 baada ya agizo malengo yalikuwa Sh1.99 trilioni na kiasi kilichokusanywa kilikuwa Sh1.67 trilioni sawa na asilimia 84.1.
Aprili malengo yalikuwa Sh1.61 trilioni ikakusanywa Sh1.34 trilioni sawa na asilimia 83.2 huku Mei ikikusanywa Sh1.33 trilioni sawa na asilimia 82 ya Sh1.619 trilioni.
“Ukusanyaji wa mapato haujashuka ukiangalia Januari wakati taskforce zinafanya kazi tulikusanya kwa asilimia 79 lakini baada ya kuzikataza Aprili tulikusanya kwa asilimia 83.2 na Mei hali nzuri kwa asilimia 82,” amesema Msigwa
Amesema Watanzania wanalipa kodi, wameitikia ulipaji kodi na ukusanyaji kodi haujaathirika kama baadhi ya watu wanavyosema
“Lakini tutoe angalizo, rais aliposema ukusanyaji wa kodi wa mabavu uachwe, kodi ikusanywe kitaalamu na kitaaluma hakumaanisha watu waache kulipa kodi. Watanzania tuendelee kulipa kodi kila mmoja mahali alipo,” amesema Msigwa
Amesema ukusanyaji mzuri wa mapato bila kutumia nguvu utaleta tija ya kupata mapato mengi zaidi kuliko kutumia nguvu na baada ya rais kuagiza vikosi kazi vilivyokuwa vinatumika kukusanya kodi vikome vimekoma havipo sasa.
“Baadhi ya vikosi kazi vile vilikuwa vinakiuka tu wanakwenda kuwanyanyasa wafanyabiashara, unawatisha na kuwanyang’anya fedha zao wakati kuna njia nzuri tu ya kukusanya kodi kitaalamu,” amesema Msigwa.