Serikali ya Tanzania yashinda kesi ya zabuni ya mafuta ICC

Muktasari:

  • ICC imeiamuru kampuni ya mafuta kutoka Falme za Kiarabu kuilipa Tanzania mabilioni ya fedha, baada ya kuvunja mkataba.

Dar es Salaam. Baraza la Kimataifa la Biashara (ICC) limeiamuru Kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC ya Umoja wa Falme za Kiarabu, kurejesha kwa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Dola milioni 9.7 za Marekani (zaidi ya Sh24.79 bilioni).

Mbali na fedha hizo, pia baraza hilo limeiamuru kampuni hiyo kuilipa PBPA fidia ya adhabu ya Dola milioni 1.14 (zaidi ya Sh2.9 bilioni) kwa kusababisha mfumo wa ununuzi wa mafuta wa pamoja kuharibika.

ICC imetoa uamuzi huo baada ya PBPA kushinda shauri la usuluhishi ililolifungua katika baraza hilo dhidi ya kampuni hiyo inayojihusha na uingizaji wa mafuta, baada ya kampuni hiyo kushindwa kusambaza mafuta kwa mujibu wa mkataba.

Shauri hilo la usuluhishi namba 2682/AZO, lilifunguliwa na PBPA kwa pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), baada ya kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC kushindwa kutekeleza mkataba wa zabuni ya uagizaji mafuta.

Kulingana na  mkataba wa zabuni namba PBPA/CPP/PMC/C3-KOJI/02/2021 wa Januari 5, 2021, kampuni hiyo ilipaswa kuingiza mafuta metriki za ujazo 36,192 ambayo yalipaswa kupokelewa kuanzia Februari 27, 2021 hadi Machi mosi, 2021.

Katika shauri hilo, pamoja na nafuu nyingine, PBPA ilikuwa ikiliomba ICC litamke kampuni hiyo ilivunja mkataba na liiamuru irejeshe fedha ilizokuwa imelipwa kwa ajili ya mafuta hayo, fidia, riba na gharama za kuendesha shauri hilo.

Taarifa ya uamuzi wa baraza hilo imetolewa Machi 9, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Prisca Ulomi, wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ICC lenye makao yake makuu Paris, Ufaransa, lililoketi hapa nchini kuendesha shauri hilo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, katika uamuzi wake uliotolewa Machi 6, 2024, limeipa ushindi PBPA na Serikali.

ICC katika uamuzi wake huo, baraza hilo limekubaliana na madai ya PBPA na Serikali na kutamka kuwa Alchemist Energy Trading DMCC ilivunja mkataba.

Pamoja na amri ya kuirejeshea PBPA fedha na fidia hiyo ya adhabu ya kuharibu mfumo wa uagizaji mafuta nchini, pia ICC limeiamuru kampuni hiyo kuilipa PBPA riba kabla ya tuzo ya asilimia 7.67 kuanzia Mei 18, 2021 hadi Novemba 2023.

Kulingana na uamuzi huo wa ICC, amri nyingine zilizotolewa na baraza hilo kwa kampuni ya Alchemist Energy ni kuilipa PBPA gharama za baraza hilo, kiasi cha Dola 882,000 za Marekani (zaidi ya Sh225.1 milioni za Tanzania).

Vile vile, kampuni hiyo ya Alchemist Energy imemriwa kuilipa PBPA gharama za kuendesha shauri hilo Sh81.28 milioni, riba baada ya tuzo ya asilimia 7.67 kuanzia siku ya uamuzi huo, Machi 6, 2024 mpaka  itakapokamilisha malipo yote.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Serikali iliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Boniphace Luhende akishirikiana na mawakili wengine kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na PBPA.