Serikali yashindwa kesi, yatakiwa kulipa fidia Sh260 bilioni

Muktasari:

  • Serikali imetakiwa kulipa fidia ya dola 109 milioni (Sh260 bilioni) kwa Kampuni ya Indiana Resources iliyoshinda kesi katika Mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji (ICSID) baada ya kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.

Dar es Salaam. Serikali imetakiwa kulipa fidia ya dola 109 milioni (Sh260 bilioni) kwa Kampuni ya Indiana Resources iliyoshinda kesi katika Mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji (ICSID) baada ya kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyosambaa mitandaoni, hukumu hiyo iliyotolewa Julai 14, mwaka huu, ambapo Tanzania imetakiwa kulipa fidia ya dola 76.7 milioni, sanjari na riba ya asilimia mbili iliyokokotolewa kuanzia Januari 10, 2018 baada ya kufunguliwa kesi hiyo, hivyo kufanya jumla ya fidia kuwa dola 109.5 milioni (sawa Sh260 bilioni kwa sasa).

"Kiasi cha tuzo hii kinaonyesha uwekezaji mkubwa ambao umepotezwa na wanahisa baada ya Serikali kutwaa Ntaka Hill kinyume cha sheria," amenukuliwa Mwenyekiti Mtendaji wa Indiana Resources Bronwyn Barnes katika taarifa yake kwa umma baada ya hukumu hiyo.

Mgogoro huo unachagizwa na marekebisho ya Sheria ya Madini ya 2017, ambayo pamoja na mambo mengine, ilifuta misingi ya kisheria ya umiliki wa leseni ya kuhodhi eneo la madini katika kipindi cha tahadhari ya biashara ya madini hayo katika soko, ili kulinda mtaji wa mwekezaji (Retention Licenses). 

Januari 10, 2018, Serikali ilichapisha kanuni za Madini (Haki za Madini), ambapo chini ya kanuni ya 21 ya kanuni hizo, Serikali ilifuta leseni zote za kuhodhi ardhi zilizotolewa kabla ya tarehe 10 Januari 2018.

Leseni hizo zilikoma kuwa na athari yoyote ya kisheria. Haki za maeneo yote yaliyokuwa chini ya leseni hizo ikiwa ni pamoja na leseni iliyokuwa kwa Indiana Resources zilihamishiwa kwa Serikali.

Kwa mujibu wa Indiana iliyokuwa ikimiliki asilimia 62.4 ya hisa za kampuni mbili za Ntaka Nickel Holdings Ltd na Nachingwea UK Limited, zilijaribu kuishawishi Serikali kurejesha leseni hiyo lakini haikufanikiwa hadi mwanzoni mwa mwaka 2020 ndipo ikawasilisha ombi la fidia ICSID.

Kampuni hizo zilifungua kesi hiyo ya ukiukwaji wa makubaliano ya mkataba wa Uwekezaji wa Tanzania (BITs) kati ya Tanzania na Uingereza chini ya uwekezaji wa kampuni hizo mbili za Uingereza.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Clay Mwaifwani ambaye ni mwanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira Tanzania (Leat), nadhani meza ya mazungumzo ndiyo suluhisho.

“Kwanza kabisa msingi wa hii kesi uko katika vilivyokuwa vifungu namba 37 na 38 kabla ya mabadiliko ya sheria ya madini na kanuni za mwaka 2018. Mabadiliko haya, yalifanya maeneo lalamikiwa kuchukuliwa na Serikali,” amesema na kuongeza;

“Wengi wa waliochukuliwa maeneo yao, walikuwa wametumia fedha zao kuyafanyia maeneo haya utafiti na walimiliki leseni halali zilizowaruhusu kufanya hivyo. Sasa hukumu hii ni pigo kwetu, pesa tunazotakiwa kulipa ni nyingi mno, na inaumiza maana zingeweza kufanya shughuli zingine za maendeleo.”

Mwaifwani ambaye amesema anaongea kama mwananchi mwenye kuumizwa na hukumu ya kesi hiyo, ametoa wito kwa Serikali kutumia ‘4Rs’ za Rais Saimia katika kutafuta muafaka nje ya mahakama.

“Wakae wazungumze na hawa watu, mazingira ya kipindi kile siyo sawa na sasa, wawaite na wakae nao meza moja. Unajua Serikali ilipoyachukuwa ilisema itafidia, na unaposema kufidia ina maana tayari unajua kuwa kuna gharama zilikuwa zimeingiwa na hao wawekezaji,” amesema na kuongeza;

“Na huu ndiyo msingi wa madai yao. Nadhani mazungumzo ni bora, tunaweza ku-negotiate na tukajikuta hatulipi kiasi hicho. Tuombe settlement ili waondoe shauri mahakamani, tutaokoa fedha nyingi, na hata wale wengine waliofutiwa, wote waitwe na tuzungume nao kabla nao hawajamua kutushtaki.