Serikali yajenga vivuko vitano, vingine vyakarabatiwa
Muktasari:
Vivuko hivyo vinavyojengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport vitarahisisha usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa visiwa vya mkoani Mwanza.
Mwanza. Serikali inatumia zaidi ya Sh20 bilioni kujenga vivuko vipya vitano vitakavyofanya safari visiwa vya Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Buchosa, Sengerema na Ukerewe mkoani Mwanza.
Akizungumza leo Jumatano Oktoba 15, 2023 wakati wa ziara ya kukagua na kujionea maendeleo ujenzi na ukarabati wa vivuko tisa unaofanywa na Kampuni ya Songoro Marine Transport, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema vitakapokamilika vitaboresha huduma ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi.
Amesema kati ya vivuko vinne vinavyokarabatiwa, kipo cha Mv Mara kilichogharimu zaidi ya Sh321 milioni ambacho kimekamilika kwa asilimia 99.
Bashungwa aliyekuwa kwenye karakana ya Songoro Marine inayojenga na kukarabati vivuko hivyo amesema hayo ni maelekezo ya Serikali kuhakikisha vivuko vyote vilivyokuwa vikitoa huduma kwa kusua sua vinakarabatiwa.
“Pia maeneo yanayohitaji vivuko vipya Serikali imetenga fedha ili vijengwe na dhamira ya Mh Rais (Samia Suluhu Hassan) anatambua nchi yetu ina visiwa na maeneo ya nchi kavu hivyo anataka kuona mawasiliano ya usafiri kwa wananchi ambao wapo kenye visiwa na sisi tunaoishi nchi kavu yanakuwa mazuri, kwahiyo nimpongeze na kumshukuru kwa kutenga fedha kujenga vipya na kukarabati vya zamani,”
Amewataka wakazi wa Musoma Vijijini kujiandaa kupokea kivuko chao akimuagiza mkandarasi kukamilisha ukarabati wake kwa asilimia 100 kufikia Oktoba 15.
“Nimejiridhisha kipo hatua ya mwisho ya kukamilika na nimuagize mkandarasi kama mkataba ulivyoelekeza itakapofika Oktoba 15, 2023 ukamilishwaji huo uwe umekamilika na Tasac asicheleweshe wananchi wa mkoa wa Mara…aje haraka iwezekanavyo ajiridhishe kama ukarabati umezingatia vigezo vinavyotakiwa ili kivuko kianze safari ya kurudi Musoma tarehe hiyo,”amesema Bashungwa huku akiipongeza kampuni hiyo kwa kazi nzuri inayofanya
Katika hatua nyingine, ameagiza ukamilishwaji kwa wakati wa vivuko vya Rugezi- Kisorya, Ijinga- Kihangara, Bwiro- Bukondo, Nyakalilo- Kome, Butagu -Mbalika, MV Nyerere na MV Kilombero alivyovikagua ili vikatoe hudma kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema uongozi wa mkoa huo utasimamia maelekezo yaliyotolewa na Serikali kuhakikisha vivuko hivyo vinakamilika kwa wakati.
“Kama ulivyoelekeza pasitokee tu urasimu wa watu fulani waje watukwamishe…nitakuja siku fulani..nitakuja..mimi naamini Songoro ameshakamilisha kazi, Tasac wakija wakamilishe yao ili yale matumaini na matarajio ya waziri aliyotoa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara basi wayapate,”amesema Makalla
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transport, Meja Songoro ameishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuwapa miradi hiyo akiahidi kuikamilisha kwa sakati na kwa ubora.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia hii miradi, tunaahidi tunaifanya hii kazi kwa weledi na uzalendo mkuibwa na tutahakikisha usiku na mchana kwamba hii miradi ikamilike kwa mujibu wa mikataba ambayo tumeiingia baina yetu na Serikali,”amesema