Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yakamilisha nyumba za watumishi Dodoma

Muktasari:

  • Serikali kupitia Wakala wa Majengo, TBA imekamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya nyumba za watumishi wa umma zilizojengwa Dodoma baada ya uamuzi wake wa kuhamia jijini humo.

Dodoma. Katika kuwaondolea adha ya makazi watumishi wa umma Serikali kupitia Wakala wa Majengo nchini, (TBA), imekamilisha ujenzi wa nyumba 150 zilizojengwa jijini Dodoma.

Hatua hiyo inakuja baada ya kuongezeka kwa mahitaji ya makazi kwa watumishi hao baada ya uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma hivyo mradi umetekelezwa kuwawezesha kuishi eneo la uhakika.

Akizungumza na Mwananchi Msimamizi wa mradi huo, Fredrick Jackson amesema mradi umetumia miezi 24 kukamilika tangu ulipoanza kutekelezwa Novemba 2021.

Jackson amesema ujenzi huo ni awamu ya kwanza ya nyumba 3500 ambazo Serikali imedhamiria kuzijenga jijini humo.

"Lengo ni kupunguza mahitaji ya makazi kwa watumishi wa umma waliohamia hapa, nyumba hizi zina gharama nafuu, mtumishi ataishi hadi pale atakapostaafu," amesema Jackson ambaye pia ni Msanifu wa Majengo wa TBA.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Dodoma, Emmanuel Wambura amesema mbali na nyumba hizo pia Wakala imeanza kujenga nyumba nyingine 150 zitakazochukua miezi 9 hadi kukamilika kwake.

Amesema vilevile kutajengwa maghorofa yenye uwezo wa kuishi familia 22 kila moja lengo likiwa ni kuwawezesha watumishi wa umma kuishi karibu na maeneo ya kazi kwa usalama na uhakika.

"TBA tumeshawapatia watumishi zaidi ya asilimia 70 wamepanga kwenye nyumba za Serikali hadi sasa katika makazi zaidi ya 6000 jijini hapa. Hivyo tunaendelea kuboresha huduma kwa watumishi hawa," amesema Wambura.

"Tulikuwa na mafundi ambao ni wa hapa hapa eneo la mradi, mama lishe, bodaboda, waliweza kupata ajira hapa na kuendesha maisha yao mbali na hayo wakazi eneo la jirani wameweza  kunufaika na maji yaliyotokana na mradi huu, pia tumejenga kituo cha Polisi," amesema.

Wakati Wambura akiyasema hayo, Elizabeth Kitwaka, ambaye ni mtumishi wa umma aliyekwisha hamia moja kati ya nyumba hizo amesema anaishukuru Serikali kupitia TBA kutekeleza mradi huo kwasababu umewaondolea kadhia ya kuhangaika kutafuta nyumba za kuishi.

Amesema mradi huo umewapa uhakika wa kuishi eneo salama na hakika tofauti na alipokuwa akiishi mtaani amesema Elizabeth.

"Tumekuwa tukihangaika huko nyuma kutafuta nyumba tena za bei ghali tunasumbuliwa na wenye nyumba ila kwa sasa tunashukuru," amesema Elizabeth.