Serikali yampa 'tano' aliyeshinda Tuzo ya Nobel

Mshindi wa Tuzo za Nobel Profesa Abdulrazak Gurnah

Muktasari:

  • Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imempongeza mshindi wa Tuzo ya Fasihi ya Nobel, Abdulrazak Gurnah pamoja na hatua ya kukitafsiri kitabu kilichompa tuzo cha ‘Peponi’ kwenda katika lugha mama ya Kiswahili.

Dar es Salaam. Oktoba 7, 2021 waandaaji wa Tuzo za Nobel walilitaja jina la Profesa Abdulrazak Gurnah mwenye asili ya Zanzibar kuwa mshindi wa tuzo hiyo kipengele cha fasihi.

Baadaye taarifa zilienea duniani kote kuhusu ushindi wa Profesa Gurnah ambaye ni mwandishi nguli wa vitabu vya riwaya aliyejikuta akipata umaarufu mkubwa kutokana na kitabu chake cha ‘Paradise’ kilichompatia tuzo hiyo.

Kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha ya Kimombo kinaelezea maisha ya Mtanzania aliyepo mazingira ya nyumbani na ugenini kilitafsiriwa na Mtanzania Dk Ida Hadjivayanis kwenda lugha mama ya Kiswahili na kuitwa ‘Peponi.

Katika kutambua ushindi wa Profesa Gurnah Serikali imempongeza Profesa huyo mwenye umri wa miaka 75 mzaliwa wa Zanzibar na kuahidi kushirikiana naye katika kuhamasisha tasnia ya uandishi nchini.

Akitoa pongezi za Serikali wakati wa uzinduzi wa riwaya hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amesema ushindi wa Gurnah unaipa chachu kuikuza tasnia ya uandishi nchini.

Profesa Nombo aliyekuwa akimuwakilisha Waziri wake Profesa Adolf Mkenda kwenye hafla hiyo fupi ya uzinduzi, amesema hata katika bajeti ya Wizara ya Elimu ya mwaka 2022/23 Serikali iliweka hela kwa ajili ya kuanzisha tuzo ya taifa ya uandishi ya Mwalimu Nyerere.

“Serikali inatambua juhudi za waandishi ndio maana ikaanzisha tuzo ya uandishi ikiwa na lengo la kukuza uandishi bunifu kukuza usomaji kuimarisha sekta ya uchapishaji kuhifadhi na kueneza utamaduni na kuimarisha matumizi ya maudhui ya Kitanzania,” amesema.

Amesema kwa mara ya kwanza tuzo hiyo ilitolewa mwaka huu na walimualika Profesa Gurnah kwa kutambua mchango wake kwenye sekta hiyo.

Akifafanua zaidi Profesa Nombo amesema kuanzishwa kwa tuzo hiyo kumeleta hamasa na imekuwa chanzo cha kuibua vipaji vya waandishi wengi.

Kutokana na hilo anaamini kuinuka kwa sekta hiyo ya uandishi kunaleta picha kwamba nchini kuna vipaji vingi kama Profesa Gurna.

Aliahidi kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha itanunua vitabu vyote vilivyochapwa nchini ikiwemo cha ‘Peponi’ na kuvipeleka kwenye maktaba mbalimbali nchini ikiwemo za shule ili visomwe watanzania wapate maarifa.

“Niwasihi tuendelee kuenzi kazi za uandishi bunifu zinazoandaliwa na Watanzania wenzetu kwakuwa tunakuza utamaduni wa kusoma pia tutakuza biashara ya uandishi uchapishaji”

Aidha aliipongeza kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota kwa kufanikisha shughuli nzima la kuchapa kitabu hicho kwa lugha ya Kiswahili.

Mshindi huyo, Profesa Gurnah amesema anafuraha kushinda tuzo hiyo kubwa duniani pia kitabu chake kuandikwa kwa lugha mama kwa mara ya kwanza ambapo watu wengi zaidi watasoma.

Gurnah amesema kilichomchochea kuwa mandishi ni kwamba hakuona maisha halisi ya Mtanzania yakiandikwa na waandishi wengine hivyo ikamchochea.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu ambaye ni mmoja wa waliohudhuria halfa hiyo ya uzinduzi, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu njia za kufanya kuiinua sekta ya uchapaji na uandikaji ili kuwapata kina Profesa Gurna wengi zaidi amesema:

“Nafikiri kuwe na namna ambayo Serikali itatoa hamasa ya watu kuandika zaidi ikiwemo unafuu wa kodi kwa wachapaji ili watu wapate nafasi ya kuandika na kuchapisha vitabu kwa urahisi.

“Ninafarijika kuona hata viongozi wetu waliotangulia wameanza kuandika kwa hiyo kumekuwa na mwamko. Nina uhakika kuna watu wengi wanaweza kuandika lakini gharama za uchapishaji zinakuwa tatizo.

Machumu amesema ili kuwekeza katika kuandika habari na hadithi za kitanzania basi kuwe na unafuu huo ili wachapishaji watachochea watu kuandika hivyo na Watanzania watasoma.