Mtanzania ashinda tuzo ya fasihi ya Nobel

Mtanzania ashinda tuzo ya fasihi ya Nobel

Muktasari:

  • Abdulrazak Gurnah, ni mwandishi nguli wa riwaya, amelitangaza vyema jina la Tanzania baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Fasihi ya Nobel kutokana na utunzi wake juu ya ukoloni mamboleo na masuala ya wakimbizi.

Abdulrazak Gurnah, ni mwandishi nguli wa riwaya, amelitangaza vyema jina la Tanzania baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Fasihi ya Nobel kutokana na utunzi wake juu ya ukoloni mamboleo na masuala ya wakimbizi.

Gurnah, ambaye alizaliwa na kukulia visiwani Zanzibar lakini akakimbilia Uingereza kama mkimbizi mwishoni mwa miaka ya 1960,
ameandika riwaya 10 ikiwamo ya “Paradise” ambayo ilichaguliwa kuwania tuzo za Booker na Whitebread mwaka 1994.

Riwaya hiyo ina marejeo dhahiri ya riwaya maarufu ya mwandishi wa Kiingereza Joseph Conrad ya mwaka 1902 “Moyo wa Giza” katika kuonyesha picha ya shujaa kijana asiye na hatia akiwa katika safari ya Afrika ya Kati na Bonde la Kongo.

Hadi kustaafu kwake hivi karribuni, Gurnah alikuwa Profesa wa Fasihi ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Kent kilichopo huko Canterbury akijikita zaidi kwa waandishi wenzake nguli kama Wole Soyinka, Ngugi wa Thiong’o na Salman Rushdie.

Mwaka jana, tuzo hiyo ilikwenda kwa mshairi wa Merika Louise Gluck.
Kabla ya kutangazwa mshindi waangalizi wa Nobel walipendekeza Chuo cha Uswidi kingependekeza na kuchagua mshindi wa uandishi kutoka Asia au Afrika, kufuatia ahadi ya kufanya tuzo hiyo kuwa tofauti zaidi.
Chuo hicho kwa muda mrefu kilisisitiza washindi wake walichaguliwa kwa sifa ya fasihi peke yao, na kwamba haikuzingatia utaifa. Lakini baada ya kashfa ya #MeToo ambayo ilitikisa chuo hicho ikisababisha kuahirisha tuzo ya mwaka 2018.

Msimu wa Nobel mwaka huu bado unaendelea huko Oslo itakakotolewa tuzo ya amani na kufuatiwa na tuzo ya uchumi.

Mkuu wa kamati ya Nobel ya Chuo cha Uswidi, Anders Olsson, alisema tafakuri ya Gurnah juu ya shida za wakimbizi ilikuwa mada tu ila
“maandishi yake yanavutia sana hivi sasa kwa watu wengi, Ulaya na ulimwenguni kote.”

Olsson alieleza hayo alipozungumza na waandishi wa habari na kubainisha kuwa madhila ya mkimbizi yanaendelea wakati wote wa kazi yake, ikilenga utambulisho na sura ya kibinafsi, pia inaonekana katika riwaya ya mwaka 1996 iitwayo “Admiring Silence” na “By the Sea” iliyotoka mwaka 2001.

Baada ya kutangazwa mshindi, Gurnal alisema wazungu wasiwaone wakimbizi kutoka Afrika kama watu waliokuja kutafuta bali wanaoweza kutoa mchango muhimu kwenye jamii hiyo mpya wanayojiunga nayo.

“Hawaji wakiwa mikono mitupu bali wenye vipaji na nguvu ambavyo wanaweza kuitumia,” alisema Gurnah.

Katika chuo kikuu anchofundisha mshindi huyo, anaelezewa anaelezewa kama msomi ambaye riwaya zake “zinarejea nyuma na kutufungua macho eneo la utamaduni anuwai la Afrika Mashariki ambalo ni geni kwa wengi katika maeneo mengine ya ulimwengu.”

Afrika haijulikani wala kufahamika kwa wengi nje ya mipaka.

Tuzo ya Nobel ya Fasihi ndiyo nishani yenye thamani zaidi duniani katika fani ya fasihi. Mbali na tuzo ya ushindi anayopewa mhusika, zawadi ya fedha taslimu takriban dola 1.1 milioni (zaidi ya Sh2.53 bilioni) hutolewa.

Gurnah ni mshindi wa tano kutoka Afrika wa tuzo hiyo hivyo anaungana na wenzake waliomtangulia akiwamo Albert Camus, Wole Soyinka na J.M Coetzee.

Vitabu vyake vingi vimekuwa vikitoa picha ya Afrika Mashariki katika kipindi cha ukoloni na hali ilivyo baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.