Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaokoa Watanzania 160 waliosafirishwa kiharamu ndani na nje ya nchi

Afisa uchunguzi kutoka sekretarieti ya kuzuia na kupambana na vitendo vya usafirishaji haramu wa binadamu, Daniel Zawadi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya Serikali katika kukomesha vitendo hivyo. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Serikali imeokoa Watanzania 160 waliosafirishwa kiharamu ndani na nje ya nchi kati ya Julai 2025 na Februari 2026, huku watuhumiwa 57 wakikamatwa. Pia imeimarisha ulinzi wa waathirika na kuendelea kutoa elimu ya kuzuia biashara hiyo haramu.

Morogoro. Serikali imefanikiwa kuwaokoa Watanzania 160 waliokuwa wamesafirishwa kiharamu kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kutumikishwa katika kazi zisizo halali, zisizo na staha na zenye ukatili, ikiwemo unyanyasaji wa kingono.

Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 9, 2026 na Ofisa Uchunguzi kutoka Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Daniel Zawadi.

Zawadi amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo maofisa wanaosimamia utekelezaji wa sheria kuhusu namna ya kuzuia, kulinda waathirika, kuendesha mashauri na kushirikiana na jamii katika kukabiliana na uhalifu huo.

Amesema waathirika hao waliokolewa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, ambapo wanawake walikuwa 96, wanaume wanne na watoto 60.

Kwa mujibu wa Zawadi kati yao, waathirika 34 waliokolewa nje ya mipaka ya Tanzania walikokuwa wamepelekwa kwa ajili ya kutumikishwa.

Aidha, amesema Serikali imewakamata watuhumiwa 57 wanaodaiwa kuhusika na usafirishaji haramu wa binadamu, huku uchunguzi na taratibu za kisheria dhidi yao ukiendelea.

"Ili kuhakikisha waathirika wa uhalifu huu wanalindwa, Serikali imeanzisha nyumba salama za kuwahifadhi wakati mashauri yao yakiendelea mahakamani.”

“Pia, imeanzisha kituo cha kupokea taarifa zinazohusu usafirishaji haramu wa binadamu na, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeendelea kutoa elimu kwa jamii ili itambue kuwa ni kosa la jinai kama yalivyo makosa mengine," amesema Zawadi.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka taasisi ya Hanns Seidel Foundation, Raphael Ami, amesema taasisi hiyo imekuwa ikiunga mkono jitihada za Serikali kupitia miradi mbalimbali inayolenga kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu.

Amesema pamoja na juhudi hizo, uelewa wa jamii kuhusu uhalifu huo bado ni mdogo, hali inayosababisha baadhi ya watu kushiriki au kushuhudia vitendo hivyo bila kutambua kuwa ni kosa la jinai.

Naye mjumbe wa Bodi ya Tanzania Relief Initiatives, Jones John, amesema mafunzo hayo yamewakutanisha mahakimu, wanasheria, askari wa Jeshi la Polisi, maofisa wa uhamiaji, ustawi wa jamii pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia, kwa kuwa ndio wanaofanya kazi kwa karibu na jamii na kusimamia utekelezaji wa sheria.