Serikali yaombwa kupunguza gharama kupanda Mlima Kilimanjaro

Wadau wa utalii wakipiga makofi wakati wa uzinduzi wa Kampeni za Twendezetu Kileleni  kupitia lango la Machame, katika kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika. Picha na Fina Lyimo.

Muktasari:

  • Serikali imeombwa kupunguza gharama ya viingilio kwa Watanzania wazawa katika kupanda Mlima Kilimanjaro ili waweze kushiriki kikamilifu maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru katika kilele cha mlima huo.

Arusha. Serikali imeombwa kupunguza gharama ya viingilio kwa Watanzania wazawa katika kupanda Mlima Kilimanjaro ili waweze kushiriki kikamilifu maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru katika kilele cha mlima huo.

Akizungumza leo Jumatatu  Novemba 13, 2023 wakati wa  ufunguzi wa kampeni ya Twenzetu Kileleni na mkurugenzi wa  Kampuni ya Africanzoom Adventure, Magreth Samson amesema Serikali kupitia wadau wake wa utalii na Tanapa/Kinapa  kuangalia umuhimu wa kupunguza gharama za kuingia hifadhini kwa wazawa.

"Tunashukuru kwa kuaminiwa, tunaahidi hapa kila atakayepanda Mlima Kilimanjaro na sisi siku hiyo kupitia lango la Machame atafika kileleni na kupata huduma zote muhimu, maandalizi yetu yapo vizuri, ili  kuhakikisha Watanzania wengi wanapanda ni vyema mamlaka zikaona namna ya kupungiza gharama za kuingia hifadhini kwa wazawa," amesema.

Ameongeza kuwa, "Tunaomba Serikali iangalie hili kwa jicho la pekee ikiwa kweli tunahamasisha utalii wa ndani, tumeshuhudia wananchi wanaotaka kupanda mlima ila gharama inakuwa kubwa," amesema Magreth.

Ameongeza kuwa katika msimu wa tatu wa Twenzetu kileleni kampuni tatu zimepata nafasi ya kuandaa na kutoa huduma ya kupanda kilele cha Mlima Kilimanjaro ambapo Kampuni ya Africanzoom Adventure imepata nafasi hiyo kwa Mkoa wa Arusha ambapo watatumia lango la Machame.

Amesema wanatarajia kupata watalii 300 ambayo watapanda kupitia lango la Machame kwa ajili ya kupandisha bendera ya taifa katika kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Joshua Nassari ameipongeza kampuni ya utalii ya Africanzoom Adventure kwa kuwa kampuni  ya kwanza mkoani Arusha kupata nafasi ya kushiriki Kampeni ya Twenzetu Kileleni kuelekea miaka 62 ya maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanganyika 9, Desemba 2023.

"Zipo kampuni nyingi za utalii ndani ya Mkoa wa Arusha ila nyie mmekidhi vigezo vilivyotolewa na Tanapa/Kinapa na mkakubali kufanya kampeni hii muhimu ya kukumbuka upatikanaji wa uhuru wetu, pokeeni pongezi nyingi kwa kuwa mnawakilisha Mkoa vizuri," amesema Nassari.

Nassari amesema kuwa kumbukumbu hiyo ni muhimu na ina weka alama ya uzalendo kwa vizazi vyote ikiwa ni pamoja na kufungua fursa ya ajira na biashara.

"Kampeni hii ni uzalendo mkubwa wa kukumbuka uhuru wetu, binafsi nina shauku ya kufika kileleni na nitapanda kupitia lango la Machame na kampuni hii," amesema Nassari.

 Mhifadhi Tanapa, Evance Magomba amepongeza kampuni hiyo kwa kupata ushiriki na kujitoa katika kuhamasisha wananchi kushiriki.

"Sisi Tanapa ‘team media’ tutapanda na Africanzoom Adventure kwa kutumia njia ya Machame, tunaamini kampuni hii itaenda kufanya vizuri," amesema Magomba.