Serikali yapiga marufuku mikopo ‘kausha damu’ mitaani, wakulima

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024 / 2025, jijini Dodoma leo Juni 13, 2024. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Wakati mikopo umiza ikiendelea kuibua vilio kila kona, wakulima nao ni miongoni mwa waliokuwa wakiumizwa kwani walikuwa wakilazimika kulipa gunia la kilo 100 baada ya kukopeshwa kilo 2 za mbegu.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ametoa onyo kwa watu binafsi na kampuni zinazojihusisha na utoaji wa mikopo inayojulikana kama ‘kausha damu’ kwa wananchi mitaani pia kwa wakulima, kuacha mara moja kwani jambo hilo linarudisha nyuma kiuchumi na kuwaingiza katika lindi la umaskini.

Dk Mwigulu amesema wapo baadhi ya watu wanaowakopesha wakulima kopo la mbegu la kilogramu 2 huku wakitaka malipo ya gunia la mazao lenye takribani kilo 100.

Malipo hayo ni sawa na riba ya asilimia 5,000 huku akitaja kitendo hicho kuwa ni dhuluma na ni wizi kama wizi mwingine.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia uwepo wa mikopo umiza inayotolewa na watu binafsi mitaani wakati akifanya uwasilishaji wa bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025.

Dk Mwigulu amesema pia wapo watu wanaokopeshana fedha kwa makubaliano ya riba ya Sh800,000 kwa mwezi ambapo mtu akikopa Sh4 milioni atatakiwa arudishe Sh28 milioni baada ya miezi 30.

“Hii ni sawa na riba ya asilimia 240 kwa mwaka. Hii nayo ni dhuluma na ni wizi kama wizi mwingine, viwango hivi ni vikubwa sana na vinawarudisha nyuma wananchi ambao wakati mwingine wanafanya makubaliano bila kuwa na elimu ya fedha,” amesema Dk Mwigulu.

Amesema jambo hilo si huruma bali ni dhuluma kwa kutumia matatizo aliyonayo Mtanzania mwingine.

“Natoa onyo kwa watu binafsi na kampuni zinazojihusisha na utoaji wa mikopo ya namna hii kuacha mara moja kwani jambo hili linarudisha nyuma wananchi wetu kiuchumi na kuwaingiza katika lindi la umaskini,” amesema Dk Mwigulu.

Amewataka wananchi kuwa na nidhamu ya fedha ikiwemo kukopa kwa ajili ya mahitaji yenye tija na ikiwezekana kuchukua mikopo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali badala ya matumizi ya kawaida.

“Pia ni vyema kuwa makini katika masharti ya mikataba ya mikopo mnayoingia na kuhakikisha mikopo mnayopewa inarejeshwa kwa wakati ili msiingie katika mitego ya wakopeshaji wenye nia mbaya ya kuuza dhamana zao,” amesema Dk Mwigulu.

Ameitaka Benki Kuu Ya Tanzania (BoT) na kamati zote za ulinzi na usalama kuendelea kufuatilia suala hili kwa ukaribu, kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaotoa huduma za fedha bila kuwa na leseni.

Pia ameagiza kuwanyang'anya leseni wote watakaobainika kuwa wanatoa mikopo bila kuzingatia masharti ya leseni na kuwaumiza wananchi.

Hata hivyo katika kutatua changamoto hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza programu ya Elimu ya Fedha kwa Umma ya mwaka 2021/22 - 2025/26 pamoja na kuhamasisha usajili na kutoa elimu ya uendeshaji wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha.

Hadi Februari 2024, Serikali imesajili jumla ya vikundi vya kijamii 49,168 vya huduma ndogo za fedha na wahamasishaji 500.

Aidha, Serikali imeteua maofisa dawati 212 katika ngazi ya wizara, mkoa, na halmashauri na kuwapatia mafunzo ya uratibu na usimamizi wa biashara ya huduma ndogo za fedha katika maeneo yao.

“Serikali imetoa leseni kwa watoa huduma za fedha daraja la pili wapatao 1,726 na vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo 759,” amesema Dk Mwigulu huku akiongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu.