Serikali yapiga marufuku mikusanyiko nchi nzima

Thursday July 22 2021
Gwajima pic
By Tatu Mohamed

Dar es Salaam. Serikali imepiga marufuku mikusanyiko yote isiyo ya lazima nchi nzima na ile ambayo itaonekena ni lazima basi tahadhari zote zichukuliwe.


Hatua hiyo inalenga kukabiliana na hofu ya kuendelea kusambaa kwa mlipuko wa tatu wa janga la corona ambao tayari umeathiri mamia ya Watanzania.


Agizo hilo limetolewa Alhamisi ya Julai 22, 2021 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ambaye amesisitiza utekelezaji wa agizo hilo.


Hata hivyo, agizo hilo limekuja wakati ambao tayari wakuu wa mikoa mbalimbali nchini, wakitangaza kupiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima kwenye maeneo yao.


Katika agizo lake hilo, Dk Gwajima amewataka viongozi wa Serikali na wa sekta binafsi kuonyesha mfano wa namna wanavyochukua hatua kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.


Dk Gwajima pia amesema kuwa mpaka sasa idadi ya wagonjwa wa Covid 19 imezidi kuongezeka na hadi kufikia Julai 21,2021 kulikuwa na wagonjwa 682 wanaopatiwa matibabu kwenye vituo mbalimbali.

Advertisement


Amesisistiza kuwa Serikali itaendelea kutoa takwimu hizo pamoja kufuatilia hali halisi ya mwenendo wa ugonjwa huo na kutangaza hatua mbalimbali za kuchukua.


“Ili kuimarisha zaidi kasi ya kuoambana na kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19, natamka kuanzia leo tarehe 22/07/2021 nimekataza shughuli zote za misongamano yote isiyokuwa ya lazima . Nimekataza shughuli zote za misongamano na ile yenye ulazima tahadhari ya kutosha ichukuliwe bila kuathiri shughuli za kiuchumi na kitaifa.


“Naelekeza wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuwapa ushirikiano waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Jamii Na. 1 ya Mwaka 2009 na kuweka utaratibu mzuri kwa wale wanaoomba vibali vya shughuli zenye ulazima,”amesema Dk Gwajima.


Pia, ametoa wito kwa wananchi wote kujiandaa kupata huduma ya chanjo kama ambavyo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alivyotangaza jana.


“Leo hii wataalamu wa afya wamekutana kupata mafunzo tayari kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa hiari na bila malipo,” amesema.

Advertisement