Serikali yapunguza viwango tozo nane za mafuta

Serikali yapunguza viwango tozo nane za mafuta

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imepunguza tozo nane za mafuta ya petroli, dizeli na taa ambazo zitawanufaisha Watanzania kwa kupunguza matumizi yafedha kwenye manunuzi ya mafuta kwa Sh102 bilioni.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imepunguza viwango vya tozo nane za mafuta ya petroli, dizeli na taa ili kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Septemba mwaka huu Serikali ilisitisha kupanda kwa bei ya mafuta nchini na kuunda tume ya kuangalia pamoja na kuchunguza ushuru na tozo mbalimbali zilizoko katika mafuta.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 5 2021 Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Godfrey Chibulunje amesema hatua hiyo imesaidia kupunguza ongezeko la bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Tozo zilizopunguzwa ni za matumizi ya miundombinu ya Bandari, tozo ya Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ya kuchakata nyaraka, Wakala wa Vipimo vya Tanzania (TBS) ya kupima ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini.

Pia Serikali imebadilisha mfumo wa utozaji wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), tozo kwa ajili ya shughuli za udhibiti za Ewura na kufuta tozo ya huduma inayotozwa katika mamlaka nne za Temeke, Kigamboni (jijini Dar es Salaam) na Tanga na Mtwara.

Nyingine ni serikali kupunguza gharama za kuweka vinasaba kwenye mafuta.

Aidha, Chibulunje amesema kutokana na kupunguza tozo hizo imesaidia kupunguza ongezeko la mafuta ya petroli, dizeli na taa.

Ametoa mfano jiji la Dar es Salaam ambalo lilikuwa iongezeke kwa Sh145 kwa lita lakini sasa itaongezeka kwa Sh 12 kwa lita.