Serikali yasaini mkataba kulipa deni la PSSSF Sh2.17 trilioni

Muktasari:

  • Wizara ya Fedha Tanzania imesaini makubaliano na Mfuko wa Pesheni kwa Mashirika ya Umma (PSSSF) ya ulipaji wa deni la Sh2.17 trilioni ambazo zitalipwa kwa utaratibu wa hati fungani maalum ya miaka nane hadi 25.

Dodoma. Wizara ya Fedha Tanzania imesaini makubaliano na MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ya ulipaji wa deni la Sh2.17 trilioni ambazo zitalipwa kwa utaratibu wa hati fungani maalum ya miaka nane hadi 25.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Jumatano Desemba 22, 2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Emmanuel Tubutu na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Hosea Kashimba.

“Baada ya kufanya uchambuzi wa kina juu ya suala hilo na kwa maslahi mapana ya wanachama wa mfuko, Serikali imeamua kulipa deni hilo kwa kuanzia Sh2.17 trilioni na deni hilo litalipwa kwa utaratibu wa hatifungani maalum ya miaka kuanzia nane hadi 25,” amesema.

Naye Kashimba amesema mkataba huo unathamani ya Sh4.66 trilioni ambao kwa kuanzia utaruhusu Serikali kutoa hati fungani zisizo taslimu (noncash bond) za thamani ya Sh2.17 trilioni za muda wa kuanzia miaka minane na kuendelea.

Amesema uwekezaji huo utasaidia mfuko kupata mapato yanayotokana na hati fungani hii takribani Sh120 bilioni kwa mwaka.