Rais Samia awasamehe wafungwa 1,082

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Kati ya wafungwa hao,  29 wamechiwa huru, 1,053 wakibadilishwa adhabu ya vifungo vyao.

Dar es Salaam. Rais Samia Hassan Suluhu ametoa msamaha kwa  wafungwa 1,082, ikiwa ni katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia ametoa msamaha huo kwa kutumia mamlaka  aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(a)-(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa msamaha kwa wafungwa kwa masharti maalumu.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, Aprili 27,2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel  Sillo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani  ya Nchi, Hamad Masauni.

Taarifa hiyo imesema kati ya  wafungwa hao waliosamehewa,  29 wameachiliwa huru tangu  jana Aprili 26,2024.

Wakati wafungwa 20  waliohukumiwa  adhabu ya kifo wamebadilishiwa  adhabu hiyo kuwa  kifungo cha maisha na  wafungwa 27  waliohukumiwa kifungo cha maisha  wamebadilishiwa adhabu na kuwa kifungo cha miaka 30.

Huku  wafungwa 1,006 wamepunguziwa adhabu zao  na watabaki gerezani  na kuendelea na sehemu ya kifungo kilichobaki.

“Msamaha huu unawahusu wafungwa ambao wamehukumiwa kifungo cha kuanzia miaka miwili na kuendelea  na ambao tayari wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na wawe wameingia gerezani kabla ya Desemba 2023,”imesehema sehemu ya taarifa hiyo.

Kigezo kingine ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua za mwisho na ugonjwa na hatua hiyo ithibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga wa Wilaya.

Wafungwa wengine ni wale wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani ambao wametumikia adhabu zao kwa miaka 15 na kuendelea  wamebadilishiwa adhabu zao kuwa kifungo cha miaka 30.

Wapo pia wafungwa wa kunyongwa waliomaliza taratibu za kimahakama ambao wamekaa gerezani kwa muda wa miaka kumi na kuendelea, ambao wamebadilishiwa adhabu hiyo na kuwa kifungo cha maisha.

“Wafungwa waliowahi kubadilishiwa adhabu kwa msamaha wa Rais  kutoka adhabu ya kifungo cha maisha ambao wametimiza miaka kumi na kuendelea tangu kupata msamaha  huo, wamebadilishiwa kifungo cha maisha kuwa kifungo cha miaka 30,”imeeleza taarifa hiyo.

Pia wapo wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi , umri huo uthibitishwe na japo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa  Mkoa au  Mkuu wa Wilaya.

Msamaha huu unawahusu wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya.

“Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi, ulemavu huo uthibitishwe na jopo  la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga Mkuu wa Wilaya.”

“Msamaha huu unawahusu  wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka kumi au zaidi.

“Ni matarajio  ya Serikali kuwa wafungwa  walioachiwa huru  watarejea  tena katika jamii  kushiriki na wananchi wenzao  katika ujenzi wa Taifa letu  na kujiepusha  kutenda makosa  ili wasirejee  tena gerezani,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.


Wafungwa wasiohusika na msamaha huo

Hata hivyo, taarifa hiyo imesema kuwa msamaha huo hautawahusu wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje na wale waliowahi kukiuka masharti ya vifungo  vya nje  chini ya sheria ya Bodi za Parole sura ya 400(R.E) 2002.

Wengine ni wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka , utakatishaji wa fedha , rushwa, usafirishaji au kujihusisha kwa namna yoyote na dawa  za kulevya ikiwemo bangi.

“Wafungwa waliopatikana na hatia ya kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho sio cha maisha  kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, unyang’anyi wa kutumia nguvu, unyang’anyi wa kutumia silaha , kumiliki silaha au ktenda makosa hayo,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ikifafanua zaidi.

“Wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali, ujangili, makosa ya wizi au ubadhilifu wa fedha za Serikali,”imeeleza taarifa hiyo.

Pia msamaha huu hautawahusu wafungwa wanaotumikia vifungo gerezani kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo.

Wafungwa wenye makosa ya kujaribu kuua,  kujiua au kuua watoto wachanga, ugaidi, uharamia na makosa ya kimtandao hawatahusika pia.

Wafungwa warudiaji na wale waliowahi kupata msamaha wa Rais , watenda makosa  ya kinidhamu gerezani ambao makosa hayo hajayatimiza miaka mitatu mpaka kufikia Aprili 26,2024  na wafungwa wa madeni, pia hawahusiki na msamaha huo.