Serikali yasitisha kulifunga Ziwa Tanganyika

Dodoma. Serikali imewaondoa hofu wananchi wa mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi kwa kusitisha kwa muda utekelezaji wa kuzuia shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu ndani ya Ziwa Tanganyika.

Uamuzi huo ulifikiwa jana kwenye kikao kilichowakutanisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Waziri Abdallah Ulega, wakuu wa mikoa mitatu, makatibu tawala, wakuu wa wilaya zinazopakana na ziwa na wataalamu wengine wa Serikali.

Kikao hicho kilifanyika kutokana na malalamiko ya wavuvi, wabunge na wadau wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, wakidai kutoshirikishwa na uamuzi wa kulifunga ziwa hilo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Ulega alifafanua kuhusu utekelezaji wa Ibara ya 14 ya itifaki inayohusisha nchi nne za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia inayozungumzia umuhimu wa kulipumzisha ziwa na shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu.

Ulega alisema Ibara ya 14 ya itifaki hiyo inazungumzia umuhimu wa kulipumzisha ziwa kutokana na shughuli za uvuvi kila mwaka kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 kwa miaka mitatu mfululizo. Lengo ni kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, katika kipindi hicho nchi wanachama wa ziwa hilo watafanya utafiti wa kiwango cha samaki, utafiti wa kibaolojia na matokeo ya kiuchumi kwa watu wanaotegemea ziwa hilo kimaendeleo.

Itifaki hiyo ilitiwa saini Desemba 2021 mkoani Kigoma na mawaziri Dk Deo-Guide Rurema (Burundi), Adrien Djema (DRC), Injinia Collins Nzovu (Zambia) na kwa Tanzania alisaini Hamad Chande aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Akizungumza baada ya mkutano huo jana, Ulega alisema wamekubali kuahirisha kwa muda uamuzi wa kuzuia shughuli za uvuvi kwenye ziwa hilo.

“Kama ilivyo kwenye taarifa yangu ya jana (juzi) ndio hivyo, hivyo tumekubaliana kuahirisha kwa muda kwa lengo la kutoa elimu kwanza,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng'enda alisema kikao hicho kiliitishwa na Ulega kwa ajili ya kushauriana juu ya mambo yanayohusu maendeleo na matumizi ya Ziwa Tanganyika.

“Mimi ninazungumza kama mwenyekiti wa mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi. Tunaishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha wananchi ambacho tulikuwa tumekileta katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kutaka kuwe na ushirikishwaji zaidi na mipango mbadala kabla ya kufunga matumizi ya Ziwa Tanganyika kwa kipindi cha miezi mitatu.

“Wamesikia kilio cha wabunge ambao tunazungumza kwa niaba ya wananchi kwa maana shughuli ya kufunga ziwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi huu hadi tarehe 15 mwezi wa nane imesitishwa na Serikali,” alisema Ng’enda.

Alisema uamuzi huo ndio uliosababisha juzi Ulega akazungumza bungeni kwamba wananchi waendelee na shughuli zao.

“Katika kikao cha leo (jana) Serikali imeendelea kusisitiza wananchi waendelee na shughuli zao wakati Serikali ikiendelea kufanya utaratibu wa ushirikishaji zaidi wa wananchi, wadau wa uvuvi pamoja na sisi wawakilishi wa wananchi, ili tuweze kupata njia bora zaidi ya kushughulika na maendeleo ya Ziwa Tanganyika,” alisema.

Ng’enda alisema wamekubaliana kukutana kikao cha pili baada ya kikao cha jana kwa lengo la kuiona mipango iliyowekwa na Serikali kwa ajili ya kuwafikia wananchi katika ushirikishaji.

Pia, alisema wataangalia njia mbadala ya kuwapatia wananchi mapato wakati ziwa litakapokuwa limefungwa kwa muda.

“Kwa hiyo tutakuwa na kikao cha pili, halafu tutakuwa na kikao cha tatu, halafu ndio tutakwenda kwenye hatua ya kuona nini kifanyike. Na wakati huo Serikali inaangalia je, ni lazima kufunga ziwa au kuna njia nyingine za kufanya mazalia ya samaki na makuzi ya samaki yafanyike bila kufunga ziwa.

“Hayo yote Serikali inakwenda kuyajadili, lakini niseme kubwa zaidi sisi wabunge tunaishukuru Serikali sikivu, kutusikia na kuahirisha kwanza jambo hili,” alisema Ng’enda.