Serikali yataja sababu za mfumuko wa bei kuongezeka

Muktasari:
Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba ametaja sababu tatu zilichochea kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini.
Dodoma. Wakati kukiwa na malalamiko ya ugumu wa maisha na kuongezeka kwa gharama za bidhaa muhimu nchini, Serikali imetaja mambo matatu yalisosababisha changamoto hiyo huku ikieleza hatua inazochukua kuleta unafuu.
Leo Juni 15, 2023 wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba, amesema miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa mfumko wa bei ni kupanda kwa gharama za bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi.
Dk Mwigulu amezitaja bidhaa hizo kuwa ni petroli, mafuta ya kula, mbolea, ngano na malighafi za viwandani huku akisema kwa umuhimu wake katika maisha ya kila siku athari zake ziligusa wengi.
Sababu nyingine iliyotajwa na Dk Mwigulu ni kupungua kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya masoko ya ndani kulikosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hususan katika maeneo yanayotegemea mvua za vuli kwa ajili ya kilimo.
“Sababu ya tatu ni kuongezeka kwa mahitaji ya chakula kutoka nchi jirani hususan ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika,” amesema Mwigulu na kuongeza kuwa nchi hizo zilizokuwa na mahitaji makubwa zililazimika kuja kununua ndani ya Tanzania
Katika taarifa yake hiyo Waziri huyo mwenye dhamana ya fedha na mipango ya nchi anasema kwa mwaka 2022 mfumko wa bei ulikuwa ni asilimia 4.3 ukiongezeka kutoka wastani wa asilimia 3.7 mwaka 2021.
Hata hivyo Dk Mwigulu amesema kiwango cha sasa cha mfumko wa bei kipo ndani ya lengo la nchi la muda wa kati na kinakidhi vigezo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) (asilimia 8) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) (asilimia 3 hadi 7).
Amesema pamoja na changamoto za athari ya mabadiliko ya tabianchi na vita inayoendelea nchini Ukraine, mwaka 2022 Serikali ilifanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuchukua hatua muhimu ikiwemo kutoa ruzuku ya mafuta na mbolea, kuimarisha usimamizi na udhibiti wa sera za bajeti na fedha hususan kutoa misamaha ya kodi, ushuru na tozo katika bidhaa za kilimo cha mazao.