Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yatenga Sh1 trilioni kujenga gridi imara ya umeme

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza leo Alhamisi, Julai 2, 2026 katika mkutano wa hadhara mkoani Mara. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

  • Dk Nchemba amesema uamuzi huo unatokana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali inayorudisha nyuma jitihada za wananchi katika kujiletea maendeleo, sambamba na kuboresha shughuli za kijamii.

Rorya. Serikali imetenga zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa gridi imara ya umeme ili kumaliza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Julai 2, 2026, na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alipohutubia mkutano wa hadhara katika Mji wa Shirati uliopo Wilaya ya Rorya, mkoani Mara.

Dk Nchemba amesema uamuzi huo unatokana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali ambayo imekuwa ikirudisha nyuma jitihada za wananchi katika kujiletea maendeleo, sambamba na kuboresha shughuli za kijamii.

Amesema baada ya uzalishaji wa umeme kuimarika nchini kutokana na kukamilika kwa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, bado kuna changamoto ya kukatika kwa umeme kutokana na gridi ya umeme kuwa na hitilafu za mara kwa mara.

“Tayari tumeimarisha uzalishaji wa umeme na umeme upo wa kutosha sasa. Huo umeme unatakiwa kutumika vema ili kuboresha uchumi wa taifa na watu wake. Kwa hiyo changamoto hii ya kukatika mara kwa mara haiwezi kukubalika, na ndiyo maana Serikali imekuja na mwarobaini kwa kujenga gridi imara ya umeme,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema Serikali inatarajia kufuta sheria ya kutaifisha mifugo katika Bunge lijalo, baada ya kubainika kuwa sheria hiyo imekuwa ikitumiwa na baadhi ya watendaji wa Serikali kwa maslahi yao binafsi na kuwanyanyasa wananchi.

Amesema utekelezaji wa sheria hiyo umegubikwa na sintofahamu nyingi, huku wananchi wakiwa ni waathirika wakubwa, hususan wafugaji ambao wamekuwa wakinyang’anywa mifugo yao kwa madai ya kuingizwa katika hifadhi za Taifa.

“Unakuta ng’ombe zaidi ya 200 wanakamatwa, na siku hiyo hiyo kesi inaendeshwa, siku hiyo hiyo mnunuaji anapatikana. Sasa unajiuliza huyu mnunuaji alijuaje kuwa siku hiyo kuna ng’ombe watataifishwa. Hatuwezi kuendelea na sheria inayowatia wananchi umaskini,” amesema.

Amesema Serikali itahakikisha inatekeleza yale yote ambayo yaliahidiwa wakati wa kampeni za uchaguzi, ikiwemo utatuzi wa changamoto za wananchi, hivyo kuwataka wananchi kutokuwa na hofu yoyote.

Kabla ya kuhutubia mkutano huo, Waziri Mkuu amepata fursa ya kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la Nyathorogo wilayani Rorya, daraja ambalo linaunganisha wilaya za Tarime na Rorya.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) Wilaya ya Rorya, Elifadhili Moses, amesema mradi huo umegharimu zaidi ya Sh729 milioni.

“Hili daraja limejengwa kwa mawe na limegharimu zaidi ya Sh729 milioni, na limekamilika ambapo hivi sasa lipo katika matazamio kabla ya kukabidhiwa rasmi serikalini na mkandarasi aliyekuwa akilijenga,” amesema Moses.

Wakizungumza kuhusu umuhimu wa daraja hilo, baadhi ya wakazi wa Kata ya Nyathorogo wamesema watu wengi wamepoteza maisha baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka eneo hilo nyakati za masika.

“Tumepoteza ndugu zetu wengi hapa, mifugo yetu pia imesombwa na maji. Tunaishukuru Serikali kwa mradi huu, sasa tunaomba na barabara ikarabatiwe ili iwe katika hali nzuri,” amesema Charles Kabwao.

Hellena Onyango amesema daraja hilo litawanufaisha zaidi wakazi wa vijiji vitano wilayani Rorya ambao wamekuwa wakitegemea kupata huduma mbalimbali, ikiwemo mnada katika eneo la Komaswa wilayani Tarime.

“Upande ule ndipo kuna mnada mkubwa wa Komaswa tunaoutegemea, lakini ukitaka kusafiri kwenda Mwanza, Musoma au Tarime lazima uvuke hapa ili kufika katika barabara kuu. Kwa hiyo kabla ya daraja hili tulikuwa tunaathirika,” amesema.

Philipo Ogodo amesema kabla ya daraja hilo walikuwa wakilazimika kutumia zaidi ya Sh10,000 kuvuka kwenda upande wa pili, lakini baada ya kukamilika kwa daraja hivi sasa wanatumia Sh2,000 pekee.

Mbunge wa Rorya, Jafari Chege, amesema jimbo hilo linakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara, ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, pamoja na ukosefu wa umeme katika baadhi ya vitongoji.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amesema Serikali inatarajia kupima vijiji vyote 6,070 nchini ambavyo havijapimwa ndani ya miaka mitano, hali ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Festo Dugange, amesema wizara hiyo imetenga zaidi ya Sh1.7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1.7 katika mji wa Shirati.