Serikali yatoa Sh10.7 trilioni ujenzi wa reli ya SGR

Miongoni mwa vichwa vya treni ya umeme ambavyo vimepokelewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kikiwa kinashushwa leo Desemba 30, 2023 katika bandari ya Dar es Salaam.

Dodoma. Serikali imeendelea kutoa fedha za utekelezaji wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) wa kilomita 1,219,  kwa kutoa jumla ya Sh10.69 trilioni na kwa ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Aprili 3, 2024 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akisoma mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/2025.

Fedha hizo ni ongezeko kutoka Sh762.99 bilioni katika bajeti ya mwaka 2023/2024 alizozitolea taarifa yake bungeni.

 “ Kama nyote mlivyoshuhudia, majaribio ya treni hiyo ya mwendo kasi yalifanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Februari, 2024. Ni matarajio yetu kuwa huduma ya usafiri na usafirishaji itaanza ifikapo Julai, 2024 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma.” amesema.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Amesema ujenzi wa Morogoro – Makutupora (kilomita 422) umefikia asilimia 96.35, Mwanza - Isaka (kilomita 341) umefikia asilimia 52.69, Makutupora - Tabora (kilomita 371) umefikia asilimia 13.86, Tabora - Isaka (kilomita 165) umefikia asilimia 5.38 na Tabora – Kigoma (kilomita 506) umefikia asilimia 1.81.

Majaliwa amesema hatua za kumpata mshauri msimamizi na mkandarasi wa ujenzi wa reli ya Uvinza – Musongati – Gitega (kilomita 282) zinaendelea.

Amesema reli hiyo ya kisasa itakapoanza kufanya kazi itarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa baina ya bandari na sehemu za ndani na nje ya nchi.

Wakati wa maombi ya fedha kwenye Bunge la Bajeti lililopita, Majaliwa alisema hadi kipindi hicho, Serikali ilitoa jumla ya Sh762.99 bilioni kutekeleza mradi huo ambapo kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (Kilomita 300) utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 97.91.