Serikali yatoa tahadhari homa ya uti wa mgongo

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Serikali imewataka Watanzania kuchukua tahadhari kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo uliotokea katika jimbo la Tshopo nchini DRC Congo.

Dar es Salaam. Serikali imewataka Watanzania kuchukua tahadhari kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo uliotokea katika jimbo la Tshopo nchini DRC Congo.

Vimelea vya ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa au kukaa na mtu mwenye maambukizi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa Septemba 8, 2021 na Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, mlipuko huo unaoambukiza ni tishio kwa sasa Barani Afrika.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Septemba 16, 2021 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale, imesema ni vyema kuendelea kuchukua tahadhari kwani magonjwa hayana mipaka, hususani mikoa inayopakana na DRC.

Dk Sichwale amesema ugonjwa huo wa mlipuko husababishwa na bakteria wanaojulikana kama ‘Neisseria meningitides’.

“Ugonjwa huu huchukua siku mbili hadi 10 tangu kuambukizwa hadi kuanza kuonyesha dalili,” amesema Dk  Sichwale.

Dalili

Dk Sichwale amesema dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na homa kali, kichwa kuuma, kutapika, kuogopa mwanga, kuchanganyikiwa na shingo kukakamaa.

Amesema ugonjwa huo unaweza sababisha madhara makubwa kwenye ubongo, kupotea kwa usikivu au ulemavu mwingine wa kudumu na hata kupoteza maisha.

“Ili kuzuia maambukizi wananchi wanapaswa kuepuka mikusanyiko ya watu wengi hasa wakati wa milipuko, makazi yazingatie mzunguko mzuri wa hewa. Hivyo wananchi wanashauriwa kutoa taarifa mapema endapo wataona mtu yeyote mwenye dalili zilizotajwa ili hatua stahiki za kudhibiti zichukuliwe mapema,” amesema.

Dk. Sichwale ameelekeza mikoa yote hususani inayopakana na DRC ikiwemo Kigoma, Rukwa, Kagera, Katavi na Songwe kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari ikiwemo kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa ugonjwa huo na utoaji taarifa kupitia mfumo wa utoaji taarifa za magonjwa ya mlipuko.

Ameitaka mikoa hiyo kuongeza nguvu ya ufuatiliaji katika mipaka, hususani kwa wageni wanaoingia nchini kutoka DRC.

“Naagiza kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa katika ngazi ya jamii hususani maeneo ya mipakani ili kutambua mapema mgonjwa na kuwaandaa watoa huduma na vituo vya huduma kukabiliana na ugonjwa huu endapo utajitokeza,” amesema.

Dk Sichwale amesema Wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa huo nchini DRC na kuchukua hatua ili kuzuia na kujiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huo endapo utajitokeza nchini.