Serikali yawaita wadau kuendelea kutoa misaada kwa waathirika Hanang
Muktasari:
- Serikali imetoa wito wa misaada zaidi ya vifaa vya ujenzi ili kusaidia waathirika kurejesha makazi yaliyoathirika.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewaalika wadau kutoa misaada zaidi ya vifaa vya ujenzi ili kusaidia waathirika na maporomoko ya matope ya Hanang, ili kurejesha makazi yaliyoharibiwa.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi, Desemba 16, 2023 na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali ikiwa ni siku 13 zimepita tangu kutokea maafa ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang wilayani Hanang mkoani Manyara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Serikali ya maendeleo ya hali baada ya maafa hayo, imesema idadi ya vifo imebakia ile ile 89, huku miili 87 ikitambuliwa na kuchukuliwa na familia zao kwa ajili ya mazishi.
Hata hivyo, miili miwili ya watoto wa kike wa umri wa mwaka mmoja na miaka mitatu inasubiri majibu ya vipimo vya vinasaba (DNA) ili itambuliwe.
Katika taarifa hiyo, Matinyi amesema idadi ya majeruhi inaendelea kupungua kutoka 139 hadi wanane waliofikishwa hospitalini baada ya maafa kutokea.
Kuhusu kampeni ya huduma za afya, Matinyi amesema wataalamu wa afya wametembelea kaya 6,640 na kuzipatia vidonge 225,975 vya kutibia maji. “Hakuna tatizo la magonjwa ya mlipuko kama kuhara au kipindupindu ambayo hushambulia maeneo ya maafa, pia jumla ya waathirika 2,496 wameshapata huduma ya afya ya akili na kisaikolojia,” amesema.
Kuhusu misaada, Matinyi amesema awali kabla ya kukatiza ziara yake ya kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP28), huko Dubai, Rais Samia Suluhu Hassan alipokea Sh2.5 bilioni kutoka kwa wahisani mbalimbali wa nje.
“Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kukusanya fedha kutoka kwa wananchi, kampuni na taasisi mbalimbali na hadi sasa imefikisha Sh218.9 milioni. Pia, taasisi na mashirika ya umma yameendelea kuchangia na hadi sasa zimefikia Sh2.2 bilioni, hivyo jumla kuu ya fedha hizi ni Sh4.95 bilioni,”
Katika ufafanuzi wake, Matinyi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Hanang pia zinaendelea kupokea misaada ya chakula, vitu na vifaa mbalimbali kutoka kwa watu binafsi, asasi, taasisi na kampuni binafsi na za umma za ndani na nje ya nchi.
“Hadi kufikia sasa misaada hiyo kwa thamani ya soko ni Sh2.18 bilioni. Vitu vyote hivi vinahifadhiwa wilayani Hanang. Juhudi zingine za Serikali za urejeshaji hali katika eneo lote lililopatwa na maafa zinaendelea,”amesema Matinyi.