Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vifo Hanang vyafika 89, miili miwili bado haijatambuliwa

Eneo la Katesh, Hanang mkoani Manyara lililokumbwa na mafuriko ambayo yamesababisha Mlima Hanang kutoa tope jingi na kusababisha maafa ya watu na uharibifu wa maji. Picha na Mohamed Hamad.

Muktasari:

  • Ni vifo vitokanavyo na maporomoko ya tope na mafuriko wilayani Hanang. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, miili miwili kati ya 87 haijatambuliwa kutokana na kuharibika

Hanang. Idadi ya vifo vilivyotokana na maporomoko ya tope,mawe na magogo kutoka mlima Hanang, imeongezeka hadi kufika 89.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Desemba 11,2023,  na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, hadi sasa miili 87 imeshatambuliwa na ndugu zao kwa ajili ya maziko.

Maporomoko hayo yaliyotokea alfajiri ya Desemba 3,2023 na kusababisha majeruhi 139,kati yao 120 walisharuhusiwa na waliobaki hospitali ni 17.

"Hadi kufikia sasa miili iliyopatikana ni 89 na miili 87 imeshatambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi. Kutokana na kuharibika vibaya, miili miwili bado haijatambuliwa,"imeeleza taarifa hiyo.

Kuhusu kambi tatu za waathirika hadi sasa zina watu 224 baada ya waathirika 98, kurejea kwa ndugu na jamaa zao.

"Serikali inaendelea na juhudi za kuunganisha waathirika na familia zao na hatimaye kuzifunga kambi. Mbali ya juhudi zote ambazo tayari zimesharipotiwa na Serikali, bado kuna kazi zaidi inaendelea ikiwemo kusafisha barabara za mitaani na vijijini na nyumba za wananchi zilizojaa tope,"imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa hadi sasa Wizara ya Afya imeshazitembelea kaya 3,993 na kutoa elimu ya afya pamoja na kugawa dawa 59,895 za tiba maji, huku wananchi 1,370 wakipata ushauri nasaha.

"Serikali inawashukuru na kuwapongeza Watanzania na taasisi mbalimbali za umma na binafsi ndani ya nchi yetu kwa moyo wa utu na uzalendo kwa kujitolea  misaada mbalimbali. Serikali inatoa wito kwa misaada zaidi ya vifaa vya ujenzi, ili viwasaidie waathirika kuanzisha makazi mapya,"imesema taarifa hiyo.