Sh1 milioni mkono wa pole kwa kila mwili Hanang

Sehemu ya nyumba za makazi ya Wananchi wa eneo la Jorodom, Katesh Wilayani Hanang likiwa tupu mara baada ya kupitiwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya matope na mawe hali iliyopelekea uharibifu unaonekana pichani.
Muktasari:
- Hadi leo Desemba 10,2023 miili 87 imeshapatikana huku majeruhi wakifikia 139,ambapo zoezi la kutafuta miili mingine bado linaendelea katika Mji wa Katesh, wilayani Hanang mkoani ManyaraHadi leo Desemba 10,2023 miili 87 imeshapatikana huku majeruhi wakifikia 139,ambapo zoezi la kutafuta miili mingine bado linaendelea katika Mji wa Katesh, wilayani Hanang mkoani Manyara
Hanang. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema licha ya Serikali kugharamia mazishi ya waliofariki katika maporomoko ya matope kutoka Mlima Hanang pia itatoa mkono wa pole wa Sh1 milioni kwa kila mwili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo, Jumapili Desemba 10, 2023 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi imesema hadi sasa miili 87 imeshatambuliwa na ndugu zao.
“Hadi kufika sasa miili iliyopatikana ni 87 na yote imeshatambuliwa na ndugu zao na kuchukuliwa kwa ajili ya mazishi na kwa maelekezo ya Rais Samia, Serikali inagharamia mazishi yote na kutoa mkono wa pole wa Sh1 milioni kwa kila mwili,”imesema taarifa hiyo
Taarifa hiyo imesema kuwa kaya 212 zipo tayari kuunganishwa na familia zao baada ya kupatiwa mahitaji muhimu ya maisha na kuwa waathirika wote 517 wameshapatiwa huduma za kisaikolojia kutokea kambini.
“Kila kaya inayoondoka kambini inapewa chakula cha siku 30 kwa kufuata mwongozo wa lishe ambao ni unga, mchele, maharage, mafuta ya kula, sukari, chumvi, maji ya kunywa, jiko la kupikia na kwa upande wa watoto wanapewa unga wa lishe.
“Kila kaya inapewa godoro, blanketi, shuka, sufuria, nguo za ndani, taulo za kike, pampasi za watoto, dawa za meno, miswaki, sabuni za miche, sahani, vikombe na vijiko,”imesema taarifa hiyo.
Huduma za jamii
Taarifa hiyo imesema katika kuhakikisha Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama imeshatembelea kaya 2,143 na kutoa elimu ya afya kwa umma na kugawa vidonge 35,154 vya kutibu maji.
Kuhusu mashamba yaliyoharibiwa, Serikali inaendelea na utambuzi ili itoe msaada wa mbegu na mbolea kwa wananchi walioathirika na kuwa hadi sasa kilo 17,000 za mbegu za alizeti, mahindi na ngano zimeshagawiwa kwa wananchi hao.
Taarifa hiyo imeeleza vifaa vya misaada mbalimbali vilivyotolewa ni mahindi kilo 47,627, maharage kilo 8,692, unga wa sembe kilo 37,745, unga wa ngano kilo 13,800, mchele kilo 39,330, mafuta ya kupikia lita 12,290 na sukari kilo 12,954,vifaa vya malazi vikiwa ni magodoro 1,920,mahema ya familia 5,
mabegi ya kulalia 600, mashuka 2,559 na maduveti 170,vifaa vingine vya matumizi ya nyumbani na mabati 5,200 ya kuwasaidia waathirika kujenga makazi mapya.