Idadi ya vifo Hanang yafikia 80

Hali ilivyo kwenye mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang' Mkoani Manyara baada ya kutokea mafuriko.
Muktasari:
- Kutokana na uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa ili kupata mchoro sahihi wa eneo lililoathirika kutoka na maporomoko ya matope wilayani Hanang, Serikali inaweka mipaka ya eneo hatarishi na wananchi ambao awali waliishi eneo hilo, hawataruhusiwa kurejea.
Hanang. Idadi ya vifo vilivyotokana na maporomoko ya matope kutoka mlima Hanang imeongezeka na kufikia 80, huku Serikali ikiweka mipaka eneo la kuepukwa, ambapo wananchi waliokuwa wakiishi hawataruhusiwa kurudi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 8, 2023 Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema, "Baada ya kufanya uchunguzi wa kisayansi wa chanzo cha janga hilo, wataalamu wa Serikali wamekamilisha kuweka mipaka eneo la kuepukwa (buffer zone) kwa kufuata mkondo wa mto Jorodom unaoshuka kutoka mlima Hanang.
“Eneo hilo ni la kati ya mita 60 na 300 kutegemeana na ardhi ilivyokaa, ambapo wananchi hawataruhusiwa kujenga makazi wala kufanya shughuli za kiuchumi katika eneo hilo kutokana na ukweli kwamba ni hatarishi,”amesema Matinyi.
Akizungumzia juu ya vifo hivyo, Matinyi amesema idadi hiyo ni ya mpaka saa sita mchana wa leo Desemba 8, 2023.
Amesema miongoni mwa marehemu hao 80 watu wazima ni 48 wakiwamo wanaume 19, huku watoto wakiwa 32 wakiwamo wa kiume 15 na jumla ya miili 79 imetambuliwa hadi sasa.
Kuhusu majeruhi, Msemaji huyo wa Serikali amesema watu 133, walipokelewa katika hospitali mbalimbali za mkoani Manyara, huku wengine 440 wanahudumiwa katika kambi za waathirika wa maporomoko hayo.
Jana Desemba 7, 2023 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama alisema idadi ya vifo ilikuwa 76.
Aidha kuhusu kuwajengea nyumba waathirika wa tukio hilo Matinyi amesema, “kwa sasa wananchi wawe na subira, mchakato na mchanganuo wa namna ambavyo Serikali itawasaidia ili kupata makazi mapya, utatolewa.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara, Matinyi amesema, “Kwa sasa kilomita 16 za barabara katika Mji Mdogo wa Katesh, zinasafishwa huku zile zinazopita maeneo ya pembezoni mwa mlima, zinafanyiwa kazi.
Imeelezwa kuwa barabara hizo za pembezoni mwa mlima, zinafanyiwa kazi kwa ushirikiano wa taasisi tatu ambazo ni Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Kwa upande mwingine bosi huyo wa idara ya Habari Maelezo, ametoa shukrani za Serikali kwa Watanzania wote waliojitolea kuwasaidia waliopatwa na janga hilo, huku akihimiza misaada hiyo ihamie kwenye vifaa vya ujenzi kwa sababu baada ya kupona watahitaji kuanza maisha mapya.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema wanaendelea kutoa elimu katika kambi na makazi ambayo hayajaathirika ili kuepusha magonjwa ya mlipuko ambapo kaya zaidi ya 750 zimefikiwa, sambamba na ugawaji wa dawa za kusafisha maji.