Serikali yaeleza wingi wa viongozi maporomoko ya Hanang, maafa yasiyozuilika

New Content Item (1)


Muktasari:

  • Serikali yaeleza maafa yaliyotokea wilayani Hanang sio la janga lisiloweza kuzuilika huku ikifafanua suala la wingi wa viongozi kwenda wilayani ikisema wote wana kazi maalumu katika kukabiliana na tukio hilo.

Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi amesema maafa yaliyotokea ya maporomoko ya matope, mawe na miti yaliosababisha vifo vya watu 69 ni tukio lisiloweza kutabiriwa kwa sababu kuna mvua za Elinino.

Matinyi amesema taarifa kutoka kwa Mamlaka ya Hali ya Tanzania (TMA), mvua zilizonyesha Desemba 2 usiku zilikuwa za kawaida na haikuleta mafuriko.

“Ni tatizo lililotekea katika mlima wenyewe wa Hanang unaotokana na chembechembe za mchanga za volcano ya miaka mingi iliyopita. Kilichotokea ile miamba laini inayotokana na mchanga wa aina hii ilivyofyonza maji na kutengeneza hali uzito na mgandamizo ambapo mlima ulishindwa kushikilia badala yake ukajiachia na tope.

“Lile tope lililojiachia likaanza kushuka chini na kuzoa miti, miamba na mawe yaliyokuwa pembeni kwa kusukuma kwa kufuata mkondo wa mto Jorodom na kusababisha madhara hasa katika vijiji vya Gendiba,” amesema Matinyi.

Matinyi ametoa ufafanuzi huo leo Jumatano Desemba 6, 2023 katika mjadala wa Mwananchi Space uliokuwa na mada ya Kama Taifa, tuna utayari kukabiliana na majanga?

Maafa hayo yaliyosababisha vifo vya watu 69 majaruhi zaidi ya 100 yalitokea Alfajiri ya Jumapili Desemba 3, 2023 katika mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya karibu vikiwemo ya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi na Sarijandu.

Chanzo cha maafa hayo ni kumeguka sehemu ya Mlima Hanang yenye miamba dhoofu iliyonyonya maji ya mvua, hivyo kuporomoko na kutengeneza tope lililokwenda katika makazi na maeneo ya biashara.

Aidha Matinyi amesema aina hiyo ya maafa ya Hanang sio tukio linaloweza kuwafundisha wananchi namna ya kupambana na maporomoko ya tope au sio aina ya tukio ambalo lingeweza kuzuilika na kamati ya maafa kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa.

“Hakuna mbinu ya kuzuia aina hii ya tukio, isipokuwa baada ya kutokea namna gani Serikali inawezi kuchukua jukumu lake la kuokoa wananchi, ndicho kilichofanyika Jumapili (Desemba 3),” amesema Matinyi ambaye ni mkurugenzi wa Idara Habari-Maelezo.

Maelezo hayo ya Matinyi ni kama vile alikuwa anawajibu wadau waliosema kwamba bado Serikali haijawa tayari kukabiliana na majanga mbalimbali wakitolea mfano maafa yaliyojitokeza Hanang wakisema walikuwa wana uwezo wa kuzuia kutokana na taarifa ya TMA.

Kuhusu wingi wa viongozi kwenda Hanang, Matinyi amejibu kuwa kila wizara iliyokwenda kwa kazi maalumu. Amezitaja wizara hiyo ni pamoja na Wizara ya Maji, Wizara ya Ulinzi akisema kuna askari zaidi ya 1,200 kwa ajili ya uokoaji na kuondoa haya matope yanabebwa kwenye malori.

“Wizara ya Afya imekuja kuhakikisha watu wote walioathirika wanatibiwa 117 ukiondoa mmoja aliyepoteza maisha, wamesharuhusiwa isipokuwa watu 41 pekee wanaoendelea na matibabu na kuhakikisha wote watakaopata tiba kiafya kutokana na kukaa pale wanahudumiwa.

“Suala la viongozi kupiga picha, wanapigwa picha siyo wanajipiga wenyewe, kiongozi hawezi kuchukua video ya siku nzima turudi kwenye uhalisia, kuanzia alfajiri hadi saa sita usiku watu wanafanya kazi, usiku huu tunazungumza mawaziri wamekaa wanajadiliana changamoto zilizopo na zilizotokea leo, kesho waamke wamezitatua,” amesema Matinyi.

Matinyi amewataka Watanzania kuacha fikra potofu kwamba majanga yatazuiliwa akisema sheria, vifaa na watu vina uwezo wa kufanya kazi linapotokea janga na majanga yanayoweza kuzuilika.

“Mfano tatizo lililopo kwenye mabonde lakini baadhi ya majanga hayawezi kuzuilika, nimedokeza kwamba wataalamu wa utabiri wanasema haikuwa mvua kubwa, huku ni kuteleza kwa ardhi kwenye mlima na kusababisha maporomoko ya matope,” amesema Matinyi