Chadema, ACT-Wazalendo wakosoa utayari kukabiliana na majanga Tanzania

Muktasari:

  • Wadau mbalimbali walioshiriki mjadala wa Mwananchi Space wamekosoa utayari wa Serikali katika kukabiliana na majanga pindi yanapotokea.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Wananchi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Suzan Lyimo ameshauri kitengo cha maafa kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu, kiondolewe na kijitegemee ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesema bado Taifa halijafanya vema katika kukabiliana na majanga hata yale yanayoweza kukabiliwa ili kuzuia vifo vya Watanzania, akitolea mfano maafa yaliyojitokeza wilayani Hanang ambayo yameonyesha kuna vifaa duni vya uokozi.

“Kikijitegemea labda kitakuwa na bajeti yake ya kutosha, kitengo cha maafa hakiwezi kuokoa watu kutokana na matukio yanayojitokeza. Serikali isifanye siasa katika maisha ya watu, lakini tuna safari ndefu katika mambo ya muhimu hasa ya kukabiliana na maafa,” amesema Lyimo.

Lyimo ameeleza hayo leo Jumatano Desemba 6, 2023 katika mjadala wa Mwananchi Space uliokuwa na mada ya Kama Taifa, tuna utayari kukabiliana na majanga?

Maafa hayo yamesababisha vifo vya watu 69 majaruhi zaidi ya 100 yalitokea Alfajiri ya Jumapili Desemba 3 katika mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya karibu vikiwemo ya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi na Sarijandu.

Chanzo cha maafa hayo ni kumeguka sehemu ya Mlima Hanang yenye miamba dhoofu iliyonyonya maji ya mvua, hivyo kuporomoko na kutengeneza tope lililokwenda katika makazi na maeneo ya biashara.

Hata hivyo, Lyimo aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu kwa miaka zaidi ya 10 amewashukuru wadau mbalimbali kwa mwamko wa waliounyesha katika kutoa michango ya kuwasaidia waathirika wa maafa hayo.

Lyimo ametoa mfano wa majanga yaliyowahi kutokea ya kuzama kwa meli ya Mv. Bukoba, Ukerewe na ajali ya ndege ya Precesion Air iliyodondoka katika Ziwa Victoria karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera.

“Kilichotokea Hanang wote tunajua kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza kuwa kutakuwa na mvua ya Elinino itakayokuwa na madhara makubwa katika maeneo mbalimbali.

“Hata kama hawajataja maeneo lakini Serikali ilipaswa kuwa na utayari wa lolote litakalojitokeza. Bado uokozi haujaridhisha, hatua vifaa vya kisasa, lakini hii misafara inayokwenda Hanang inakwenda kufanya nini?

Naye, Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu aliungana na Lyimo akisema Taifa halijawa tayari kukabiliana na majanga, licha ya TMA kutoa taarifa mapema ya tahadhari.

“Majanga yanahitaji kuwa na maandalizi ya watumishi, vifaa, miundombinu lakini umma wenyewe wa Watanzania wapewe mbinu za kujiokoa. Idara hii ya maafa ingekuwa na mpango mkakati wa kueleweka unaoenda na hali halisi ya sasa sambamba na teknolojia tungeokoa maisha ya watu.

“Haya majanga yanayojitokeza sijui moto au Hanang unaona kabisa tunafanya uokozi usiokuwa na dira, hatujui tunapoelekea,” amesema Semu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, bara.

Kwa upande wake, mtalaamu wa majanga, Boniface Jacob amesema mkakati ya udhitibiti wa majanga wa miaka mitano 2022/2027 umetoa namna nzuri ya kushughulikia majanga kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Ukisoma Watanzania walioandika mwaka jana ndiyo walioandika mwaka huu na ndiyo walewale waliopo Hanang, walikubaliana kutengeneza kamati za kukabiliana na majanga na walisema zitashuka hadi kwenye kamati za vijiji kuanzia kurasa za 65 na wameelezea kwamba itaanzia juu kwa Waziri Mkuu na itashuka kwenda kwenye Wizara.

“Kama kweli wangetekeleza hicho walichoandika kwenye mpango mkakati yasingetokea haya tunayoongea leo, tatizo limetokea usiku lakini Serikali imefika… Kitu pekee ninachoshauri tuseme inatosha vifo vilivyotokea inatosha ifike hatua Serikali izindue hivi vituo vya maafa ili janga lolote likitokea hao watumike itasaidia, tuna vikosi vya jeshi ambavyo ndiyo kazi zao waje wale, siyo wanakuja wa aina nyingine,” amesema Jacob