Ma-RC watakiwa kujipanga kukabiliana na majanga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama akizungumza na wanahabari leo Jumamosi Desemba 9,2023 mji mdogo wa Katesh, mara baada ya kupokea misaada ya vifaa vya ujenzi kutoka kwa wadau wa maendeleo. Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Wakuu wa mikoa 14 iliyotajwa kupitiwa an mvua za El-Nino wametakiwa kujipanga kukabilianana majanga na kuimarisha ulinzi wa mali. Pia wametakiwa kuhakikisha kwanza wanaokoa wananchi ili kuzuia vifo.
Hanang. Serikali imewaagiza Wenyeviti wa Kamati za maafa za mikoa yote nchini kujipanga na kuhakikisha janga linapotokea wanachukua hatua za haraka ikiwemo kuokoa maisha ya watu.
Agizo hilo limetolewa leo Desemba 9,2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, mjini Katesh baada ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo vya ujenzi na dawa kutoka kampuni ya Multicables Ltd (MCL) na Dhehebu la Bohora, vyenye thamani ya Sh70 milioni.
Amesema kila Mkuu wa Mkoa hasa katika mikoa 14 ambayo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilisema mvua za El-Nino zitaathiri mikoa hiyo na kusababisha mafuriko,maporomoko ya ardhi,upotevu wa mali na madhara kwa binadamu na mazingira.
Amesema wakuu wa mikoa hiyo wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha hakuna uharibifu mkubwa wa miundombinu, badala yake waimarishe ulinzi wa uhai wa wananchi.
Amesema utabiri unaonyesha hali ya hewa itaendelea hivi hadi Januari, na kuwa jana katika maeneo mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam kumetokea mafuriko,daraja limeharibika ila kamati ya maafa imekesha hapo kuhakikisha hali inarejea katika hali yake ya kawaida.
"Kwa ile mikoa 14 tunashuhudia matukio ya namna moja au nyingine niendelee kutoa wito kwa kamati za maafa za mikoa na wilaya nchini kote zijipange pindi maafa yanapotokea na pale wanapozidiwa kama ilivyotokea Hanang, kamati ya maafa ya Taifa tuko tayari kusaidia,"amesema.
"Na bahati nzuri Ofisi ya Waziri Mkuu ilishafanya vikao na semina elekezi na kupeana mkakati wa namna ya kufanya pale majanga yanapotokea, miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhakikisha huduma za kijamii kama maji safi na salama,afya,miundombinu,umeme,hazikosekani.
"Niwapongeze Dar es Salaam, kamati ya maafa ya mkoa ilikesha kwenye daraja kuhakikisha wanarudisha mawasiliano,tumeona Kahama (Shinyanga) nao wameendelea,nitoe wito mkoa wa Mbeya nao wawe makini,"amesisitiza Waziri Jenista
Kuhusu waathirika wa maporomoko ya matope kutoka Mlima Hanang, amesema kwa sasa wanaendelea kusafisha baadhi ya mitaa na kujipanga kwa ajili ya upatikanaji wa makazi ya kudumu ya waathirika hao.
"Tumeona hapa mmetuletea vifaa vya ujenzi tunashukuru sana kuna miundombinu ya Serikali imepata madhara sana, tumeshaanza kufanya kazi na kuirejesha katika hali yake,mmetuletea mabomba ambayo pia yatatumika kwa waathirika watakapokuwa wanatengeneza makazi ya kudumu," amesema.
Kuhusu soko la Mji mdogo wa Katesh amesema wamefanya tathmini walichogundua kuna mkondo mpya wa asili wa maji unapita katikati ya soko, hivyo watakaa na wataalamu kuangalia kama eneo hilo litakuwa salama.
"Tutaangalia kisha tutatoa maoni na mapendekezo ya Serikali na nini kifanyike, tumeenda pale maji yote yanayoendelea kutiririka toka mlimani yanapita katikati ya lililokuwa soko,tunakamilisha kusafisha mitaa, mtaa wa kuelekea sokoni ulikuwa unatusumbua sana tope lilikua jingi,lina maji halichoteki halibebeki.
"Tushukuru sana vikosi vya ulinzi na salama leo tumefanikiwa kutoboa mitaa iliyokuwa haiwezekani na tutaamini ule wa sokoni utafunguka leo na ndiyo uliokuwa na stoo za kuhifadhi vyakula,mji ulikosa mahali pa kununua chakula lakini leo tunaamini tutafungua na shughuli zitaendelea,"amesema.