Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuwajengea nyumba waathirika Hanang

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 10 Desemba, 2023 mara baada ya kupokea hundi ya michango kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya Maafa ya maporomoko ya ardhi Hanang

Muktasari:

  • Ni wale ambao nyumba zao zilibomolewa na maporomoko ya matope katika eneo la Katesh, Hanang wiki iliyopita.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa tumaini jipya kwa waathirika wa mafuriko wilayani Hanang, akibainisha kwamba hakuna kitakachoizuia Serikali kuwajengea nyumba za Sh25 milioni au Sh30 milioni ili warudishwe kwenye maeneo yao.

Rais Samia amesema mahitaji ya wathirika wa mafuriko hayo ni mengi ikiwamo ya nyumba, vifaa vya ndani ya nyumba yakiwemo magodoro na mahitaji ya watoto ya shule.

"Wale watu siku nimeonana nao kambini walisema tumebakia sisi tu, mwingine alikuwa na mume kaachwa na watoto, lakini waliniambia mashamba na vijumba vyetu vyote vimeondoka nikatoa ahadi kwao.”

"Niliwambia hakuna atakayebaki na shida," amesema Rais Samia jana wakati akipokea hundi ya Sh2 bilioni ambayo ni michango ya Taasisi za Umma kwa waathirika hao”.

Rais Samia ameagiza kutengenezwa kijiji cha wathirika, akitaka michango yote itangazwe kwa umma na ijulikane nani kapeleka kitu gani.

"Tunahesabu kwa vidole, kama Sh5 bilioni tunataja, lakini kuna ile huyu kapeleka roli la maji na nini, yote tuiweke kwenye orodha ili tuwatangazie umma nani kapeleka nini?," amesema Rais Samia akisisitiza fedha iliyotoka ikafanye yaliyokusudiwa na kuwapa faraja waathirika.

Rais amegusia wanaoishi mabondeni wanapaswa kuhama badala ya kusubiri hadi wafikiwe na majanga kisha kuisema Serikali ambayo ilishawapa tahadhari.

"Hili ni kusudi, miezi miwili kabla ilitangazwa kuwepo kwa mvua kubwa juu ya wastani, kuna ile kawaida yetu ya kusubiri hadi tuone, kuna watu wako mabondeni wanasubiri hadi kufikiwa kisha wanasema Serikali hii ni kusudi.”

"Tulisema mapema mitaro izibuliwe ili maji yakija yaende, hakukuwa na ufuatiliaji, pia kuna wananchi wana tabia ya kusubiri mvua kubwa wanatupa taka kwenye mitaro, hizi ndiyo zinaleta mafuriko.”

"Ukitenmgeneza kwako unampa maafa mwenzako, hivyo mikoa, wilaya na Halmashauri tusimamie hayo,  mvua zinyeshe maji yapite, tumeanza kujenga mabwawa ya kukinga haya maji, kwingine bado, lakini tujipange haya maji yasituletee athari," amesema Rais.

Amesema kama nchi imepata hasara ya kupoteza maisha ya watu na mali kule Hanang, lakini hatujaomba msaada toka nje.

"Yote tumeyafanya toka hapa ndani na kimya kimya tunamaliza, juzi nilisema tuna michango nje, walituchangia dola 1milioni kwa huruma lakini hatukuomba, hatusemi kwamba hatutaomba siku zote. na Mungu atuepushe na majanga makubwa zaidi," amesema.

Rais Sami amesema mchakato wa mashirika ya umma kuchangia ulipoanza, alijua ni mzigo mkubwa na hali ya mashirikia ilivyokuwa.

"Nikasema mmmhh! Huu ni mzigo mkubwa, lakini sasa onyesha mashirika yanajua yanakaa kibao gani na njia zake ni zipi, huu ndiyo umuhimu wa kuwa na mashirika ya umma, lazima yaguswe yajue yamekaa pale kwa ajili ya umma

"Niliona orodha ya mashirika 270, mengi changua viwango tofauti, yanayojiweza yalichangia hadi Sh50 milioni, yapo ya Sh20 milioni na Sh10 milioni, mengine hadi Sh2 milioni, kilichonipa faraja zaidi katika matukio kama haya yangesubiri Serikali tuseme changeni basi, lakini mmejisukuma wenyewe."

Rais Samia ameeleza namna alivyoagiza Ofisi ya Waziri mkuu ikamilishe tathimini kwa kuwa zoezi la sensa limetoa taarifa nzuri hivyo wakamilishe tathimini ili wajue nini kinakwenda kufanywa kwa waathirika hao na warudishwe kwenye maeneo yao.

Awali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia jana Jumamosi, Desemba 9, 2023 asubuhi vifo 87 vimeripotiwa kutokea.

Amesema majeruhi 139 wanaendelea kuimarika na ambao wako hospitali ni 30 huku 19 wakiwa  hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, wanane wanaendelea kutibiwa katika hospitali ya Wilaya ya Tumaini na watatu wako kwenye kituo cha afya Gendabi

"Kaya 107 zimepoteza makazi mpaka sasa, tulipata kaya nyingi za kutosha, lakini mifumo yetu ya kieletroniki imebaini nyumba zote zilizoathirika, bahati nzuri zoezi la sensa la mwaka 2022 limeonyesha kila kitu na wamiliki wa nyumba wameonekana.

"Watu 322 ndiyo waathirika  kwenye hizi kaya 107, sasa yule atakayezungumza idadi kubwa tutazungumza naye kama sensa ilionyesha ana ng'ombe 100 leo aseme alikuwa nao 1000 tutazungumza naye," amesema.

Amesema wamewashirikisha wana kaya na wenyeji waliopo kwenye maeneo hayo, ingawa pia kwenye maeneo ya Ganana na Katesh kuna nyumba zilikuwa na wapangaji nao wameorodhesha kwani nao ni waathirika na Serikali itawahudumia.

"Lazima tutengeneze makazi ya watu 322, kama kaya ilikuwa na nyumba ya watu 10, watapata makazi ya idadi hiyo ili kuwaondoa waathirika kwenye makambi, utaratibu unaendelea vizuri kwenye makambi yote matatu.

"Hadi sasa (jana mchana) hatuna malalamiko makubwa na wananchi, hatuna malalamiko na wadau wala taasisi kwa kuwa tumejipanga vizuri kwenye uratibu," amesema Waziri Mkuu.

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema wamekusanya Sh2.1 bilioni ambazo jana walikabidhi hundi ya Sh2 bilioni kwa Rais Samia.

"Hii Sh100 milioni nyingine iliendelea kuchangwa baadae, pesa hii ipo tunasubiri kuelekezwa iingizwe kwenye akaunti ya maafa au vinginevyo,” amesema Mchechu