Serikali yawatoa hofu sekta binafsi nishati safi

Kamishna msaidizi wa maendeleo ya umeme, Styden Rwebangila akifungua mjadala wa wadau wa sekta ya nishati kujadili mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya wizara kwa mwaka 2022/2023.
Muktasari:
- Wadau wa sekta binafsi wakutana kujadili na kutathmini mwelekeo wa sekta baada ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 sambamba na changamoto zilizopo na namna ya kukabiliana nazo.
Dodoma. Wizara ya Nishati imewahakikishia wadau wa sekta binafsi kuwa Serikali inathamini mchango wa matumizi yote ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo umeme, gesi na nishati nyingine zote rafiki kwa mazingira na afya.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Juni 10 jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, Styden Rwebangila alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba kwenye mjadala wa wadau wa sekta ya nishati.
Wadau hao wamekutana kujadili na kutathmini mwelekeo wa sekta ya nishati, baada ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 sambamba na changamoto zilizopo na namna ya kukabiliana nazo.
"Napenda kuwatoa hofu wadau wa sekta binafsi na Watanzania kuwa nishati safi ya kupikia inajumuisha nishati zote na si gesi pekee kama wengine wanavyodhani," amesema Kamishna Rwebangila.
Amesema Wizara ya Nishati inathamini mchango unaotolewa na wadau wa maendeleo, hususan Umoja wa Ulaya kwa kufadhili miradi mbalimbali kwenye sekta ya nishati, hususan nishati safi ya kupikia.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana nao katika upangaji wa mipango mkakati na uendelezaji wa sera.
Naye Meneja Mradi wa Nishati kutoka Umoja wa Ulaya, Massimiliano Pedretti, amesema Umoja wa Ulaya utaendelea kufadhili miradi ya nishati safi ya kupikia kupitia mfuko maalumu wa nishati safi, kulingana na mkakati na utekelezaji wa kufikia azma ya asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo 2034.
Pedretti amesema ili Tanzania ifikie azma yake, ni lazima ichukue jitihada za makusudi kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wauzaji wa mitungi ya gesi na watengenezaji wa majiko ya umeme, ikilenga kuchochea wananchi kutumia nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu na upatikanaji wa haraka.
Mradi wa mfuko maalumu wa nishati safi ya kupikia unafanya kazi na Wizara ya Nishati kuhakikisha taasisi kama magereza, shule na hospitali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zinaweka miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Matumizi Bora ya Umeme kutoka Shirika la UNDP, Aaron Cunningham, amesema UNDP iliamua kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania kwenye sekta ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha pia inaanzisha programu hiyo, ili kuwe na matumizi bora ya nishati ya umeme kwenye vifaa vitakavyotumiwa na wadau.
“Tayari wameshaainisha viwango vitakavyotumiwa kwenye bidhaa tano kama vile vipoza umeme, jokofu, televisheni, feni na majiko ya umeme ili vitumie umeme kidogo,” amesema Cunningham.
Amesema mradi huo unatekelezwa kwa pamoja na Wizara ya Nishati tangu ulipoanzishwa mwaka 2022 na wamekuwa bega kwa bega na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili viwango hivyo vitoe unafuu wa matumizi ya umeme kwenye vifaa hivyo.