Serikali yazungumzia samaki waliokutwa wamekufa ufukweni

Thursday July 22 2021
samaki pc

Biashara ya samaki soko la feri jijini Dar es Salaam

By Anna Potinus

Dar es Salaam. Serikali imewataka wafanyabiashara wa samaki katika masoko ya Jiji la Dar es Salaam kuendelea na biashara zao kama ilivyo kawaida wakati uchunguzi ukiendelea kufanyika kufuatia vifo vya samaki walionekana kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Aga Khan jana Jumatano Julai 21, 2021.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini inasema baada ya tukio hilo, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), maofisa uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa na meneja wa soko la Magogoni Feri walikusanya samaki kiasi cha Kilogramu 164 na kufikisha Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.


“Baada ya kutolewa kwa ufafanuzi wa hali iliyojitokeza ilikubaliwa kuwa sampuli za samaki hao zichukuliwe kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kubaini sababu za vifo vya samaki hao.


“Sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya maabara ya TAFIRI, maabara ya Taifa ya Uvuvi na Polisi Kitengo cha Sayansi ya Uchunguzi kwa ajili ya kupeleka maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali,

"kiasi cha Kilogramu 156 kilichosalia kilikabidhiwa kwa ofisa uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuteketezwa na tukio la kuteketezwa lilishuhudiwa na maofisa wa wizara, uongozi wa Soko la Feri, ofisi ya uvuvi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,” imesema taarifa hiyo.

Advertisement