Prime
Setting tano muhimu kuifanya betri ya simu yako isichoke haraka
Muktasari:
- Kitendo cha kuacha huduma zisizo muhimu kwenye simu zikiendelea kufanya kazi kinaweza kuchosha betri ya simu yako.
Dar es Salaam. Malalamiko ya betri kuisha haraka ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili watumiaji wengi wa simujanja.
Wapo wanaolazimika kuchaji mara mbili au zaidi kwa siku, jambo linaloweza kuathiri mawasiliano, kazi na matumizi ya kawaida.
Hata hivyo, kitaalamu mara nyingi tatizo hilo halisababishwi na betri kuharibika, bali na mipangilio ya simu ambayo huachwa ikiwa imewashwa bila ulazima.
Kwa mujibu wa Google, mfumo wa Android umeboreshwa kwa vipengele vinavyoweza kusaidia kuongeza muda wa matumizi ya betri ikiwa vitatumika ipasavyo.
Kwanza: Washa Adaptive Battery. Hiki ni kipengele kinachotumia akili unde (AI) kujifunza programu unazotumia mara nyingi na kupunguza matumizi ya programu ambazo huzitumii.
Kwa kufanya hivyo, simu hupunguza matumizi ya nguvu bila kuathiri utendaji wa programu muhimu.
Kipengele hiki hupatikana kupitia Settings > Battery > Adaptive Battery.
Tumia Battery Saver
Ikiwa unajua hutapata nafasi ya kuchaji simu kwa muda, tumia Battery Saver.
Huduma hii hupunguza shughuli zinazofanyika nyuma ya pazia, kama vile kusasisha (updates) programu na baadhi ya huduma za eneo (Location). Matokeo yake ni kuongeza muda wa betri kwa saa kadhaa zaidi.
Punguza mwangaza wa skrini (Brightness level)
Kwa kuwa skrini ndiyo hutumia sehemu kubwa ya nguvu za betri, unapaswa kupunguza mwangaza au kutumia Adaptive Brightness, jambo linaloweza kuongeza muda wa matumizi ya betri bila kuathiri matumizi ya kawaida.
Kutumia Dark Mode, hasa kwenye simu zenye skrini za OLED, kunaweza pia kusaidia kupunguza matumizi ya umeme.
Unapaswa kuzima huduma usizozitumia. Bluetooth, GPS na Wi-Fi zinapotumika bila sababu huendelea kutumia nguvu ya betri.
Ni vyema kuzizima pale ambapo hazihitajiki na kuziwasha tu unapozitumia. Hatua hii pia husaidia kuboresha usalama wa simu.
Unapaswa kuangalia programu zinazotumia nguvu kubwa ya betri kupitia sehemu ya Battery Usage. Android huonyesha programu zinazotumia nguvu nyingi kuliko nyingine.
Ukigundua programu isiyo muhimu inatumia betri kupita kiasi, unaweza kuizuia kufanya kazi kwenye background au kuifuta kabisa.
Mambo yanayoharibu betri ni pamoja na kuacha simu ikiwa kwenye jua kwa muda mrefu, kutumia chaja zisizo rasmi, na kucheza michezo mizito wakati simu inachaji.
AI imeanza kusaidia matumizi ya betri
Katika matoleo mapya ya Android, Google imeongeza matumizi ya AI ili kutambua tabia ya mtumiaji na kupunguza matumizi ya nguvu pale inapowezekana.
Mfumo huo hujifunza programu zinazotumika mara kwa mara na kupunguza shughuli za zile zisizotumika, jambo linalosaidia kuongeza muda wa betri bila mtumiaji kufanya marekebisho mengi.
Ushauri kwa watumiaji
Wataalamu wanashauri watumiaji wasiwe na haraka ya kubadilisha betri au kununua simu mpya kila wanapoona betri inaisha haraka.
Badala yake, waanze kwa kukagua mipangilio ya simu, kufanya masasisho ya mfumo na kuondoa programu zisizo muhimu.
Kwa kufanya hivyo, inawezekana kuongeza muda wa matumizi ya betri kwa kiasi kikubwa na kuboresha utendaji wa simu bila kutumia gharama yoyote.