Sh1.7 bilioni kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, kuendeleza miradi
Moja ya miradi ya Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) inayotekelezwa katika Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya kupitia Ofisi ya Rais – Mazingira.
Muktasari:
- Mradi huo unalenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kuboresha miundombinu ya mifugo na kuibua miradi ya kiuchumi itakayosaidia kupunguza migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji wilayani Mbarali.
Mbarali. Serikali imetoa zaidi ya Sh1.7 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya, ukiwa na lengo la kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kutoa suluhisho la kudumu kwa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Kupitia mradi huo, Serikali pia inawekeza katika miradi ya kuongeza thamani ya mazao na mifugo, ikiwemo ujenzi wa viwanda vidogo vya kuchakata mafuta ya alizeti na kusindika maziwa katika Kijiji cha Matebete.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kuwezesha wafugaji kuendesha ufugaji wa kisasa unaozingatia sheria, kanuni na matumizi bora ya rasilimali za ardhi na maji.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Juni 5, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo yenye changamoto za matumizi ya ardhi.
Amesema kwa Mkoa wa Mbeya, mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri za Mbarali na Mbeya Vijijini kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
“Uhifadhi wa mazingira hauwezi kufanikiwa bila kushirikisha jamii inayozunguka maeneo husika, lakini baadhi ya wananchi wanafanya shughuli zinazohatarisha mazingira, ikiwemo ukataji miti, uvamizi wa vyanzo vya maji na matumizi yasiyo endelevu ya ardhi,” amesema.
Historia ya migogoro Mbarali
Mweli amesema kwa miaka mingi Wilaya ya Mbarali imekuwa ikikabiliwa na migogoro ya wakulima na wafugaji inayotokana na ushindani wa matumizi ya ardhi, malisho na vyanzo vya maji.
Amesema wafugaji wengi wamekuwa wakihamahama kutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao, hali iliyosababisha mifugo kuingia kwenye mashamba ya wakulima na wakati mwingine kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji.
“Unapomzungumzia mfugaji, maisha yake yanategemea mifugo. Ili iendelee kuishi ni lazima apate malisho, lakini wakati mwingine hali hiyo husababisha uvamizi wa maeneo ya kilimo na maji, jambo ambalo limekuwa chanzo cha migogoro ya muda mrefu,” amesema.
Kwa mujibu wa Mweli, changamoto hizo zilifanya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira kuona umuhimu wa kuanzisha miradi itakayowawezesha wananchi kiuchumi na kutoa suluhisho la kudumu.
Amesema badala ya wananchi kutegemea shughuli zinazochochea uharibifu wa mazingira, mradi huo umeweka mkazo katika uwekezaji wa miradi ya kiuchumi itakayoongeza kipato na kutoa ajira.
“Lengo ni kujenga uchumi wa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye migogoro. Wanapopata fursa za kiuchumi wanapunguza utegemezi wa shughuli zinazoharibu mazingira na hivyo migogoro nayo inapungua,” amesema.
Mweli amesema Serikali inaamini kuwa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, Mbarali itaendelea kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji huku wananchi wakinufaika na fursa mpya za uzalishaji.
Miradi iliyotekelezwa
Amesema mradi wa SLR umeanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2023/24 na hadi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali imenufaika na zaidi ya Sh1.7 bilioni.
Fedha hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya zao la alizeti na kusindika maziwa, pamoja na miradi mingine ya kuboresha sekta ya mifugo.
“Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira aliweka mawe ya msingi ya miradi hiyo inayotekelezwa kupitia programu ya SLR,” amesema.
Ametaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifugo, majosho ya kuogeshesha mifugo sambamba na kuweka miundombinu itakayorahisisha shughuli za wafugaji na kupunguza changamoto za kimazingira.
Mbarali kuimarisha zao la alizeti
Mweli amesema halmashauri hiyo imeanza kuweka mkakati katika uzalishaji wa alizeti kama zao mbadala la kibiashara litakaloongeza kipato kwa wananchi na kupanua wigo wa uchumi wa wilaya hiyo.
“Tumezoeleka zaidi kwa kilimo cha mpunga, lakini sasa tunataka kuona zao la alizeti linakuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa wananchi, na ndiyo lengo la kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya zao hilo,” amesema.
Amesema katika kutekeleza miradi hiyo, halmashauri imechangia Sh15 milioni ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo chanya kwa wananchi na mazingira rafiki.
Mkazi wa Kata ya Madibira, Wilaya ya Mbarali, Amos John amesema uwepo wa mradi huo utasaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Tunaona matokeo makubwa ya Serikali katika kutatua migogoro kwa kuwekeza miundombinu ya kisekta, jambo ambalo litaifanya Wilaya ya Mbarali kupiga hatua mbalimbali, hususan katika uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya alizeti na maziwa,” amesema.