Sh10 bilioni zajenga maabara ya mionzi

Muktasari:
- Serikali imetumia zaidi ya Sh10 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa maabara Changamano katika Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania iliyopo Jijini Arusha kwajili ya kuimarisha upimaji wa vyanzo mbalimbali vyenye mionzi.
Dodoma. Serikali imetumia zaidi ya Sh10 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa maabara Changamano katika Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania iliyopo Jijini Arusha kwajili ya kuimarisha upimaji wa vyanzo mbalimbali vyenye mionzi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni Mosi, 2021 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara hiyo.
Profesa Ndalichako amesema maabara hiyo pia itasaidia kuendeleza matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia katika maendeleo.
Waziri Ndalichako amesema maabara hiyo itakuwa na maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanyia tafiti, kuendeleza teknolojia na matumizi ya nyuklia.
Amesema maabara hiyo itasaidia kuangalia viasili vya mionzi kwenye vyambo mbalimbali vikiwemo vinavyotokana na huduma za tiba.
“Maabara hii ikikamilika itakuwa kati ya maabara tano bora Afrika, katika maabara hii kutakuwa na kitengo cha kufanya tafiti kuangalia mionzi inayoweza kutumika katika tiba kwa ajili ya wagonjwa wa saratani,” amesema Ndalichako katika taarifa iliyotumwa na kitengo cha mawasiliano serikalini cha wizara hiyo.
Akiwa katika Tume hiyo pia amezindua rasmi Bodi mpya ya taasisi hiyo yenye wajumbe 9 inayoongozwa na Mwenyekiti Profesa Joseph Msambichaka.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC Profesa Msambichaka amesema katika utekelezaji wa majukumu yao itatoa kipaumbele kusimamia ukamilishaji kwa wakati ujenzi wa jengo la maabara Changamano ili liweze kuhudumia Watanzania na nchi za jirani kwa viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume za Nguvu za Atomiki nchini Prof. Lazaro Busagala amesema jengo hilo litakuwa na maabara nane, maabara za kupima viasili vya mionzi.
Maabara nyingine ni za uchunguzi na utafiti wa viasili vya mionzi kwa ajili ya matibabu ya saratani, maabara ya utengenezaji vifaa vinavyotumia vifaa vya mionzi au vifaa vya nyuklia, maabara ya upimaji wa viwango vya mionzi kwenye simu na minara ya simu.