Sh14.04 trilioni mifuko ya hifadhi zawekezwa kwenye miradi

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobasi Katambi

What you need to know:

  • Mfuko wa hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unaongoza kwa uwekezaji ambapo hadi sasa wamewekeza Sh7.49 trilioni kati ya Sh14.04 trilioni zilizowekezwa na mifuko yote.

Dodoma. Mfuko wa hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unaongoza kwa uwekezaji ambapo hadi sasa wamewekeza Sh7.49 trilioni kati ya Sh14.04 trilioni zilizowekezwa na mifuko yote.

Katika hesabu zilizokaguliwa hadi Juni 30,2022 na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliwekeza Sh6.03 trilioni wakati mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF) una jumla ya uwekezaji wa jumla ya Sh521.9 bilioni.

Majibu hayo yametolewa bungeni leo Mei 16,2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobasi Katambi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Halima Mdee.

Mbunge huyo ametaka kujua tangu kuanzishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ni kiasi gani cha fedha kimewekezwa na kila mfuko na nini faida na hasara za uwekezaji huo.

Katambi amesema faida za uwekezaji ni kulinda thamani ya michango ya wanachama na kuhakikisha mifuko inakuwa endelevu ili kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulipa mafao.

“Aidha uwekezaji huu huchangia pia kuongeza ajira, mapato ya Serikali kupitia kodi na kuchochea shughuli za uchumi,” amesema Katambi.

Hata hivyo Naibu Waziri amesema katika uwekezaji wowote kuna vihatarishi (risk) ambavyo vinaweza kusababisha hasa kwa baadhi ya uwekezaji.

Ametaja hasara zilizojitokeza kwa uwekezaji uliofanywa na mfuko ni pamoja na kutolipwa kwa wakati mikopo iliyotolewa kwa wanufaika na baadhi ya miradi kutofanya vizuri ikilinganishwa na matarajio yaliyokuwepo wakati wa kubuni miradi hiyo.