Mdee awavaa Bawacha, wenyewe wamjibu

Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee.

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee amesema wanawake wa baraza walioandama kupinga yeye na wenzake, kuondolewa bungeni, ni watoto wa juzi na hawajui alikotoka.

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), wakiandamana kina Halima Mdee waondolewe bungeni, mbunge huyo amesema hao ni ‘watoto wa juzi na hawajui alikotoka’.

 “Unajua watoto hawatakiwi kunyimwa usingizi, ndio maana siwajibu wengi wanaopiga talalila ‘kelele’ wamenikuta mjomba napiga mzigo pale (Chadema). Wametamani baada ya mzigo kutema, ukishakuwa mkubwa huwezi kuangaika na watoto, wanasema unawaacha,”amesema Mdee.

Mdee aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Bawacha kwa nyakati tofauti ameeleza hayo leo Jumanne Mei 16, 2023 wakati akihojiwa na Wasafi TV jijini Dodoma. Katika maelezo yake, Mdee amesisitiza kuwa yeye bado ni Chadema ‘for life’.

Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge amemjibu kwa kusema sio sahihi kuzungumza kauli kama hizo, hata hivyo, akasema waswahili wana msemo unaosema ‘mfamaji haishi kutapa tapa.’ Ruge amedai Mdee ameonyesha dharau kwa Bawacha kusema waliondamana ni watoto.

“Katika yale maandamano kulikuwa na kina mama ambao Mdee aliwakuta katika chama, wakiwemo Mama Kimaro, Suzan Kiwanga, Grace Kiwelu na Lucy Owenya, Je wakati huo wangesema yeye mtoto hafai kuwa mbunge angejisikiaje?  tunaona ni dharau,”amesema Ruge.

Mei 11, mwaka huu viongozi wa Bawacha na wanachama wengi wa Chadema walifanya maandamano yaliyoanzia Posta ya zamani hadi ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam, kushinikiza Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuwaondoa wabunge 19 waliofukuzwa uanachama na kupoteza sifa ya kuwa wabunge.

Maandamano hayo yamefanyika wakati kesi ya wabunge hao kupinga kuvuliwa uanachama ikiendelea katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, ambapo inatarajiwa kutajwa tena hapo kesho Mei 17.

Mbunge huyo, aliyewahi kuhudumu ubunge wa jimbo la Kawe kwa miaka 10, amesema yeye ni Chadema ‘for life’, akisema inawezekana kuna watu hawataki arudi katika chama hicho, lakini watake wasitake yeye bado ni Chadema.

“Mimi ni Chadema ‘for life’, tunawasiliana na Chadema seniors (waandamizi), alisema Mdee ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Alipoulizwa kuhusu Serikali kutumia fedha kuwalipa yeye na wenzake 18 wanaodaiwa kuwa hawapo kihalali bungeni, Mdee alisisitiza kuwa wapo kihalali bungeni, ndio maana suala lao lipo mahakamani.

“Hivi kweli wakili makini na matata kama Peter Kibatala, hivi kunaweza kusiwe na zuio la mahakama, halafu mahakamani kukapoa? sio rahisi, ni maneno ya barabarani huwa sipendagi kuangaika nayo, ningehangaika nayo leo ningekuwa chizi,”amesema Mdee.

Mdee na wenzake 18 walivuliwa uanachama wa Chadema Novemba 27, 2020 baada ya kubainika katiba na kanuni za chama hicho kwa uamuzi wao wa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa Viti Maalum bila chama hicho kuwapitisha.

Mbali na Mdee, wengine ni Grace Tendega, Esther Matiko, Ester Bulaya, Cecilia Pareso, Hawa Mwaifunga, Jesca Kishoa, Nusrat Hanje, Kunti Majala, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.