Kesi ya kina Mdee, wenzake 18 yashindwa kuendelea

Baadhi ya Wanachama wa Chadema wakiwemo wajumbe wa Bodi ya  Wadhamini wa Chama hicho, Ruth Mollel (katikati) na Dk Azaveli Lwaitama (kulia) wakitoka Mahakama Kuu, baada ya kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama  inayowakabili walikuwa Wabunge 19 wa chama hicho, akiwemo Halima Mdee, kuahirishwa.

Muktasari:

  • Leo kesi hiyo ilipangwa kuendelea kuhojiwa kwa maswali ya dodoso kwa Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Chadema imeshindwa kuendelea kutokana na Jaji aliyepangwa kusikiliza kesi hiyo kuwa na majukumu mengine.

Dar es Salaam. Kesi ya waliokuwa wanachama wa Chadema iliyofunguliwa na Halima Mdee na wenzake 18 wanaopinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho, imeshindwa kuendelea katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam.

 Sababu ya kuahirishwa kwa kesi hiyo ni Jaji anayesikiliza shauri hilo, Cyprian Mkeha kuwa na majukumu mengine nje ya ofisi.

Mdee aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dar es Salaam, wakipinga kufukuzwa uanachama kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).

Kesi hiyo ilipangwa leo April 18, 2023 kwa ajili ya kuendelea kuhojiwa kwa mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Chadema, Ruth Mollel.

Kutokana na hali hiyo, Msajili Wa Mahakama Hiyo, Veronica Mteta ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 17 na 18, 2023 itakapoendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mawakili wa pande zote mbili kuitwa 'chember Court' na kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili Peter Kibatala amedai kuwa kesi hiyo imeahirishwa mbele ya Msajili Wa Mahakama hiyo, Veronica Mteta.

"Msajili Wa Mahakama hii, Veronica Mteta ametuita (mawakili wa pande zote mbili) chumba namba 76, kama mlivyoona na kutueleza kuwa jaji ana majukumu mengine nje ya ofisi na kisha kuiahirisha kesi hii hadi Mei 17 na Mei, 18, 2023 ambapo itaendelea" amedai Kibatala.

Baada ya taarifa hivyo kutolewa na Kibatala, wanachama na wafuasi wa chama hicho walishuka chini kutoka ghorofa ya kwanza walipokuwa wamekaa wakisubiri kuingia mahakama ya wazi na kisha kuondoka katika viunga vya Mahakama hiyo.

Hata hivyo, taarifa nje ya mahakama zinaeleza kuwa kuna mkutano mkuu wa mwaka wa Majaji nchini nzima, unaoendelea jijini Mwanza.

Tayari Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Dk Azaveli Lwaitama ameshahojiwa maswali ya dodoso na Wakili Ipilinga Panya anayewatetea Halima Mdee na wenzake.

Miongoni mwa ushahidi alioutoa mahakama hapo, Dk Lwaitama alipohojiwa maswali ya dodoso Machi 9, 2023, alidai kuwa wakati wa utawala wa hayati Rais John Pombe Magufuli Mamlaka zilikengeuka.

Akizungumzia kuhusu taratibu za kutangaza wabunge baada ya uchaguzi, Dk Lwaitama alidai katika mazingira ya kuaminiwa ya kawaida ambayo sio ya mwaka 2020 ni Spika wa Bunge baadaa ya kupokea majina Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

"Katiba ya Jamuhuri ya Muungano naiheshimu ndio maana nashangaa kuna watu walioko bungeni (kupitia jina la chama hicho), ziko mamlaka kwenye chama zilishautaarifu umma kuwa taratibu za kuteuliwa wabunge hazikufuatwa na sisi tukapata taharuki,"

Alidai kuwa wakati waleta maombi hao wakitangazwa yeye alikuwa Bukoba, hivyo alisikia kwenye vyombo vya habari ikiwemo magazeti wakiapishwa Jambo lililoibua taharuki.

Kuhusu wito kwa waleta maombi hao kwenye kikao cha kamati kuu alidai, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika aliwaita kupitia vyombo vya habari na njia ya Tehama (ujumbe kwa whatsup)

Alipoulizwa tuhuma zinazowakabili akidai waleta maombi hao walienda kuapa, chama kikiwa hakijawateuwa wala kupeleka majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

"Mamlaka ina jukumu la kupeleka majina, aliyewaita kwenye kikao alikuwa ameshatangaza hakuna majina yaliyopelekwa na watu waliona,"

Kuhusu mamlaka za nidhamu alidai kila mahali pana utaratibu wake wa kuwajibishana endapo mtu amekosea hata kwenye chama kuna taratibu, katiba na kanuni hata kikundi kina utaratibu wake.

 "Ninachofahamu kama mwana falsafa, kama raia kuna taratibu na kwenye kikundi pia kuna taratibu zake.

Alisema kwa yeye binafsi anaweza kujiondoa kama anabanwa, wanapotaka kushughulikia jambo la nidhamu linatokana na katiba, kanuni na miongozo.

 "Kwa upande wa chama yapo mambo tunayokubaliana, kuna mamlaka sijawahi kuwa sehemu ya hizo mamlaka, hakuna sula la nidhamu lisilo na mamlaka na usipofuata huo utaratibu unatengwa,"alidai.

Dk Lwaitama ambaye ni mwananchama wa Chadema tangu mwaka 2015 alifafanua kuwa kama mamlaka ndio yenye jukumu la kusema flani kafanya kitu flani atengwe.

 "Mtu kama umejiunga kwenye kikundi flani na wenye mamlaka wakasema umekiuka uondoke una haki ya kuondoka,"

Kuhojiwa kwa wajumbe hao wa bodi ya wadhamini Chadema kunatokana maombi yaliyowasilisha mahakamani hapo awali, baada ya kupokea kiapo cha mjibu maombi namba moja ambaye ni bodi ya wadhamini ya Chadema).

Mbali na Dk Lwaitama wajumbe wengine wanaotarajiwa kuhojiwa ni, Silivester Masinde, Ruth Mollel, Mary Florian Joachim, Francis Joseph Mush, Maulida Anna Komu na Ahmed Rashid Hamis.

Katika kesi hiyo Wabunge hao wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022, kutupilia mbali rufaa zao za kupinga uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 27, 2020 kuwafukuza uanachama kwa tuhuma za kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya Chama.