Siasa bila vurugu ndani ya maridhiano
Dar es Salaam. Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) na kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan mjini Moshi mkoani Kilimanjaro yametoa taswira mpya ya siasa za Tanzania, kwamba zinaweza kufanyika kwa mazungumzo bila vurugu.
Nyuso za bashasa zilitawala katika Ukumbi wa Kuringe mjini Moshi ulipofanyika mkutano huo, wakati viongozi wa Chadema na Rais Samia walipotoa hotuba zilizosheheni maudhui ya maridhiano ya kitaifa.
“Nilipopata mwaliko wa kuja kwenye maadhimisho haya sikusita kwa sababu nikiwa Rais wa Tanzania kundi hili (wanawake) ni langu, pia huwezi kuitwa na wananchi wako ukasema siji.
“Nilifurahi kuja kwa sababu nilijua leo nitapata fursa ya kusikia Chadema wanasema nini na nimewasikia,” alisema Rais Samia baada ya kusikiliza hotuba za viongozi wa Bawacha na Chadema.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Samia, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alieleza jinsi vyama vya upinzani vilivyopitia nyakati ngumu miaka kadhaa iliyopita.
“Kwa mazingira ya kawaida, Serikali na chama chako kingepaswa kuliomba radhi Taifa letu, kwa namna ambavyo tulipitishwa katika miaka kadhaa,” alisema Mbowe.
“Yawezekana (Rais) hukuhusika moja kwa moja, lakini tusiukatae ukweli kwamba chama chako kimeliumiza Taifa na kimeumiza Watanzania kwa njia mbalimbali,” alisema.
Hata hivyo, alisema: “Sisi kama Chadema tumekuwa tayari kusamehe, tuko tayari kusamehe na kusahau tulikotoka kwa sababu Mheshimiwa Rais umeonyesha roho nyepesi, roho ya wazi, roho safi ya kulibadilisha Taifa na kujutia huko tulikotoka”.
Ilipofika wakati wa kutoa hotuba yake, Rais Samia naye alieleza ugumu wa kufikia maridhiano, ikiwa ni pamoja na ndani ya chama chake, CCM.
“Wakati tunajadiliana kuhusu kuruhusu mikutano ya hadhara ndani ya chama changu halikuwa jambo rahisi, maana kuna wahafidhina kama ambavyo wapo hata ndani ya Chadema,” alisema Rais Samia.
Kuunganisha Taifa
Akizungumzia namna alivyoweza kutekeleza kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake mwaka huu inayogusia masuala ya ubunifu, Rais Samia alisema baada ya kuingia madarakani alikuja na ubunifu wa kuliunganisha Taifa na ameamua kufanya hivyo kwa kushirikiana na vyama vyote vya siasa.
Alisema: “Tulianza na ngazi ya kwanza kwa vyama vya siasa kupitia taasisi zao wakae watuambie changamoto ni nini, chama chenu hiki kikasema hapana, mnataka kusikilizwa peke yenu.
“Haikuwa rahisi, lakini nikasema haya nitawasilikiza peke yao, nikamwagiza makamu mwenyekiti aunde timu yake ya watu watano na mwenyekiti wa Chadema timu yake ya watu watano, nikasema wakae wazungumze.
“Tumezungumza na katika mazungumzo yale yapo ambayo tumeshayafanyia kazi na mengine tunaendelea kuyafanyia kazi”.
Alieleza mazungumzo hayo ndiyo yamemwezesha kupata fursa ya kuwa mgeni rasmi na kuzungumza na wanawake wa Chadema, jambo ambalo halikuwa rahisi hapo awali.
Kauli hiyo ilipokewa kwa shangwe na wanawake zaidi ya 3,000 waliohudhuria kongamano hilo na kusababisha ukumbi mzima kulipuka kwa vigelegele na kumwimbia wimbo ‘mama mamaa huyo mamaa’.
Rais pia alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi pamoja, akisema: “Twendeni tukafanye kazi kwa pamoja kukuza uchumi wetu, kustawisha jamii yetu ya Kitanzania na kukuza siasa zetu, tufanye siasa za kistaarabu si za kulumbana. Panapotokea hoja tukae tuzungumze na si kupayuka kwenye majukwaa tukaanza kushambuliana.”
Hata hivyo, alisema utamaduni wa kukaa chini na kuzungumza si jambo rahisi kwa watu wengi na unakuwa na vikwazo kwa pande zote mbili za mazungumzo, akisema wapo wasiotaka mazungumzo hayo kufanyika.
“Najua hili si rahisi kwangu, kuna vikwazo hata huko kwenu, huwa napitia maoni yetu Jamii Forum nasoma nacheka, najisemea huu ni utamaduni mpya, si rahisi kukubalika kwa haraka lakini wakiona matunda yanayotokea utamaduni huu utakubalika.”
Pia Rais aligusia kaulimbiu ya Chadema ya “No hate No Fear (Hatuna chuki wala woga) kuwa ni jambo jema kutolipiza visasi.
“Leo nimemsikia Mbowe anasema Chadema wamewafundisha watu wake hakuna haja ya kulipiza kisasi, nimefurahi sana na hiyo ndiyo kuvumiliana,” alisema.
Hata hivyo, alisema awali alipoanza hatua hizo alipata upinzani.
“Nilipopendekeza kwenye chama changu tufufue mikutano ya hadhara kulikuwa kugumu, mjadala ulikuwa mkubwa kama mnavyofanya nyie, najua Mbowe juzi alishambuliwa kwa nini amemuita Rais kwenye hili jukwaa.
“Kwa hiyo mwenyekiti wale wahafidhina wapo kwangu na kwako pia,” alisisitiza.
Mchezo wa siasa
Katika kuwatania Chadema, Rais Samia alisema siasa ni mchezo wa fikira na mawazo kubishana kwa hoja, huku kila upande ukiwa na lengo la kushika dola.
Hata hivyo, alisema “kwa sura ninazoziona hapa hamna dhamira ya kushika dola 2025, mnajua mama yupo, dhamira hiyo haipo. Sawa, wote tuna dhamira hiyo lakini tukafanye kwa ustaarabu,” alisema.
Katiba mpya
Mapema, Mbowe alizungumzia kilio cha muda mrefu cha Katiba mpya, suala ambalo pia lilijitokeza hata kwenye nyimbo na hotuba za viongozi wa Bawacha.
Mbowe alimtaka Rais Samia kutopuuza suala hilo, akisema ndiyo kilio cha Taifa kwa sasa huku akimsihi aone umuhimu wa kuongeza kasi ya mchakato huo.
“Ulitangazia dunia kuwa unakwenda kuunda chombo kitakachoratibu Katiba mpya, muda umekwenda kidogo ni miezi miwili sasa, tunatambua majukumu makubwa yanayokukabili, lakini vilevile ona jambo hili nalo linahitaji umuhimu wa kipekee,” alisema Mbowe.
Naye Rais Samia akijibu suala hilo, alisema chama chake hakipingani na hitaji hilo la Katiba Mpya kwa kuwa hata chenyewe kinaona umuhimu wake na hivi karibuni kwa kushauriana na vyama vya siasa kamati hiyo itatangazwa kushughulikia suala hilo.
Kuhusu tume huru ya uchaguzi, Mbowe alimtaka Rais kutoruhusu kwenda katika uchaguzi mkuu ujao (2025) na mifumo na watu walewale walioiletea Tanzania aibu kwenye macho ya dunia.
“Tukubali kama Taifa kusema kwa pamoja never, never, and never again. Maisha tuliyoishi kwa miaka sita labda wenzetu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mnaona kwenu ni utani, hamjui namna wenzenu tuliishi na roho tumezikamata mikononi,” alisema Mbowe.
Alisema inawezekana ndani ya chama na Serikali kuna wahafidhina wanaotamani kukwamisha maridhiano au mchakato wa kuipata Katiba mpya, ikiwemo Tume huru ya uchaguzi kwa kisingizo cha kulinda CCM, watu ambao alisema hawaitakii mema nchi.
“Nakusihi, nakusihi, nakusihi usikubali dhambi hiyo, kwani adhabu anayotoa Mungu wetu hatutamani imkute mtu yeyote katika nchi yetu.”
Wabunge 19
Katika hatua nyingine, Mbowe pia alizungumzia suala la wabunge 19 wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee ambao alisema walipelekwa bungeni na vyombo vya Serikali bila kupitishwa na chama hicho, akimtaka Rais kuhurumia kodi za wananchi maskini zinazowalipa mishahara wabunge hao.
Alisema licha ya kesi kuwa mahakamani na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutambua kuwa hakuna zuio la mahakama linalowapa wabunge hao uhalali wa kubaki bungeni, wameendelea kuachwa.
“Angalia wabunge wa viti maalumu Mheshimiwa Rais, ni watu wanatokana na kundi la kinamama ambalo ni jeshi kubwa ndani ya chama, hawa wote hawana uwakilishi kabisa ndani ya Bunge kwa sababu kuna watu 19 ambao mfumo wa Serikali yako na spika wako mmeamua kuwalinda ndani ya Bunge,” alisema
Hata hivyo, Rais Samia hakutaka kujihusisha na suala la wabunge hao kwa sasa, akisema: “Tuache mkondo uendelee, tutazame yanayokuja na si rahisi mimi kutia mkono,” akimaanisha kuingilia uhuru wa mahakama.
Demokrasia si chaguo
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema demokrasia haipaswi kuwa na chaguo, hivyo ni ya lazima na hakuna Taifa lililoipuuza na kukumbatia udikteta likastawi.
Alisema kama nchi inapaswa kuwa na viongozi ambao wakati wote wana hofu ya Mungu na viongozi waliochaguliwa kihalali kupitia chaguzi huru, haki na kwa uwazi.
“Kuna kauli ya miaka mingi ya kifilosofia inayosema kauli ya wengi ni sawa na kauli ya Mungu, viongozi wanapopata kura nyingi za halali kutoka kwa wananchi wanakuwa wamepata kibali cha Mungu wetu,” alisema.